MFUMO WA VIFURUSHI VYA BIMA YA AFYA WAZINDULIWA RASMI...ELIMU KUTOLEWA NYUMBA KWA NYUMBA

Mfumo wa vifurushi vya Bima ya Afya umezinduliwa rasmi jana jijini Dar es Salaam, huku Mwenyekiti wa Bodi ya Mfumo wa Bima ya Taifa (NHIF) Anna Makinda, akisema watu watafuatwa mpaka majumbani kupewa elimu ili wajiunge.

Makinda ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge, aliwataka pia watumishi wa vituo vya afya na hospitali, kuwa na lugha nzuri kwa watu wanaotumia bima hizo.

Alisema kuna baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa hawatoi kipaumbelea kwa watu wanaotumia bima ya afya na kuwataka waache tabia hizo.

“Utoaji wa huduma za afya sasa unaenda kwa ushindani, hospitali yenye wahudumu wa afya wanaotoa huduma nzuri ndio watakaopata fedha nyingi, mtu akiumwa atatamani kwenda kwenye hospitali inayotoa huduma nzuri.

“Wahuduma waendelee kuwa na bidii, kuna baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa na lugha chafu kwa wagonjwa hasa wanaotumia bima, hawa nawaambia waache tabia hiyo wagonjwa, wanahitaji lugha zenye faraja.

“Uzinduzi huu unaenda na ile azima ya Tanzania ya viwanda, utakuwa na msaada katika kuleta  afya njema kwajamii kwani bila afya njema hakuna uchumi wa viwanda, hivyo ni msaada mkubwa kwa wananchi wote, watumishi watapita majumbani kutoa elimu ya vifurushi hivi ili watu wengi wajiunge,”alieleza Makinda.

Kutokana na baadhi ya watu kuamini kuwa kukata bima ni kupoteza fedha, Makinda aliwaomba Watanzania waweke kipaumbele katika kupata bima ya afya kwa hiyari ili kuepuka gharama kubwa wanapougua.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post