MEYA WA ARUSHA KUPITIA CHADEMA KALISTI LAZARO AJIUNGA NA CCM

Wakati kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zikiendelea nchini, aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha Kalisti Lazaro amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa na Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.



Ndugu Kalisti Lazaro aliyefika katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam ameeleza amefikia uamuzi huo baada ya kupitia wakati mgumu akiwa katika Wadhifa wake wa Meya wa Jiji la Arusha.

Ndugu Kalisti amesema amepokea barua za maonyo mara kadhaa kutoka Uongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambazo zilimtaka kutokutoa ushirikiano na Viongozi wa Serikali ambao anatakiwa kufanya nao kazi ngazi ya Mkoa na Wilaya na kutompongeza hadharani Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo ameifanya Nchini ikiwamo katika Mkoa wa Arusha.

Vitisho vya mara kwa mara ikiwamo dhidi ya uhai wake ndio vimepelekea kujivua nafasi zake zote katika Chadema na kujiunga na CCM, Chama ambacho kinashughulika na utatuzi wa kero za wananchi. 

Ndg. Lazaro pia amechukizwa na Chama chake kujitoa katika uchaguzi huku akiita kitendo hicho uvunjaji wa demokrasia ambacho ndani ya masaa mawili uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema iliwanyima mamilioni ya wapenda demokrasia haki ya kushiriki katika Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.

Ndg. Kalisti Lazaro amesema sasa yuko tayari kuchapa kazi ya wananchi akiwa ndani ya Chama ya Mapinduzi na kwamba yuko tayari kwa maelekezo ya kazi kutoka Uongozi wa CCM.

Ndg. Kalisti kwa kujiunga na CCM amejiuzuru nafasi ya Udiwani, Umeya wa Jiji la Arusha, Uenyekiti wa Mameya na Madiwani wote wa Chadema Nchini na Ujumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Ndugu Kalisti Lazaro atapokelewa rasmi na wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha katika tarehe itakayopangwa hivi karibuni.

Imetolewa na,

IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527