MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI YA SERIKALI 2020/21 WAWASILISHWA BUNGENI


UTANGULIZI
1.            Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kutoa ushauri kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa  na Serikali katika mwaka wa fedha 2020/21 na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21.


2.            Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema ambayo imetuwezesha kukutana tena hapa Jijini Dodoma kwa ajili ya kutekeleza majukumu muhimu ya kikatiba ya Muhimili huu wa Bunge kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Vile vile, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu umoja, na amani ambavyo vimekuwa nguzo muhimu ya kutuwezesha sisi watanzania kuendelea kutekeleza majukumu yetu, kila mmoja kwa nafasi yake, na kuchangia katika ujenzi wa Taifa.

3.            Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufikisha umri wa miaka 60 tangu kuzaliwa kwake. Tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia afya njema na maisha marefu zaidi ili kutuwezesha watanzania wote kufurahia mafanikio makubwa ambayo yanaendelea kupatikana chini ya uongozi wake mahiri. Hakika tunajivunia kumpata kiongozi mchapakazi, mzalendo, anayechukia rushwa, mtetezi wa wanyonge na mfano wa kuigwa barani Afrika.

4.            Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kuendelea kuliongoza Bunge hili Tukufu kwa weledi mkubwa katika kuishauri na kuisimamia Serikali. Aidha, napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kwa ushauri mzuri waliotupatia wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa kuanda Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata (2020/21).

5.            Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa fedha 2020/21 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali yanawasilishwa katika Bunge lako Tukufu kwa mujibu wa Kanuni ya 94 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016. Mapendekezo haya ya Mpango na Mwongozo yameainisha vipaumbele na masuala muhimu ya kuzingatiwa na Maafisa Masuuli wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma wakati wa kuandaa, kutekeleza, kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji  wa Mipango na Bajeti za Mafungu yao.

6.            Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21 yamezingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 - 2020/21); Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; Sheria ya Bajeti, Sura 439; Sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya kisekta na kikanda (EAC, SADC na AU); na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

7.            Mheshimiwa Spika, masuala yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21 ni pamoja na:

A.           MWENENDO WA VIASHIRIA VYA UCHUMI

8.            Mheshimiwa Spika, uchumi wa Taifa umeendelea kuwa imara ambapo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita (2009 – 2018), Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.4 kwa mwaka. Katika mwaka 2018, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2017 kwa mwaka wa kizio wa 2015. Aidha, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019 (Januari – Juni), Pato la Taifa kwa mwaka wa kizio wa 2015 lilikua kwa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa uwekezaji hususan katika ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege; kutengamaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Sekta zilizokua kwa kasi zaidi katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019 ni pamoja na ujenzi (asilimia 16.5), uchimbaji madini na mawe (asilimia 13.7), habari na mawasiliano (asilimia 10.7), maji (asilimia 9.1) na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (asilimia 9.0). Aidha, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 3.6 mwezi Agosti 2019 na kuendelea kupungua hadi asilimia 3.4 mwezi Septemba 2019.

9.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Juni 2019, urari wa malipo ya kawaida ulikuwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 2,257.3 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 1,771.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2018, sawa na ongezeko la nakisi kwa asilimia 27.4. Hii ilitokana na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, hususan, bidhaa za kukuza mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa hapa nchini. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha na kukidhi mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa na huduma nje ambapo hadi Agosti 2019, akiba ya fedha za kigeni (bila kujumuisha bidhaa na huduma ambazo zinalipiwa na fedha za uwekezaji wa moja kwa moja) ilifikia dola za Marekani milioni 5,200.1, ikiwa ni sawa na uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 6.0. Ujazi  wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 27,163.2 Agosti 2019, sawa na ongezeko la asilimia 8.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Mwenendo wa viashiria vya sekta ya kibenki ulikuwa wa kuridhisha ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa faida kutokana na uwekezaji wa rasilimali kutoka asilimia 6.88 Agosti 2018 hadi asilimia 8.16 Agosti 2019 na kuongezeka kwa faida kutokana na uwekezaji wa mtaji kutoka asilimia 1.68 Agosti 2018 hadi asilimia 1.89 Agosti 2019. Kwa ujumla gharama za mikopo zilipungua ambapo riba za mikopo zilifikia wastani wa asilimia 16.77 Agosti 2019 kutoka asilimia 17.09 Agosti 2018. Aidha, mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kukua na kuchochea shughuli za kiuchumi ambapo hadi Agosti 2019 ukuaji ulifikia asilimia 8.2 ikilinganishwa na asilimia 5.2 Agosti 2018.

10.         Mheshimiwa Spika, mwenendo wa thamani ya Shilingi uliendelea kuwa tulivu katika kipindi cha mwaka unaoishia Agosti 2019, ambapo Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,289.1 ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,273.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Deni la Serikali lilifikia shilingi bilioni 52,303.04 Agosti 2019 ikilinganishwa na shilingi bilioni 49,283.44 Agosti 2018. Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2018, inaonesha kuwa Deni la Serikali bado ni himilivu katika muda mfupi, wa kati na mrefu kwa vigezo vya kimataifa.

11.         Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi yanapatikana katika Sura ya Pili ya Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango na Sura ya Pili katika Sehemu ya Kwanza ya kitabu cha Mwongozo.

B.           UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19

12.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 mapato ya ndani yalifikia shilingi bilioni 18,529.6 sawa na asilimia 88.7 ya lengo la shilingi bilioni 20,894.6. Kati ya kiasi hicho, mapato yaliyokusanywa na TRA yalikuwa shilingi bilioni 15,511.3, mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 2,356.9 na mapato ya Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 661.4. Kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato kulichangiwa na upotevu wa mapato kutokana na shughuli za magendo, hususan kupitia bandari bubu katika ukanda wa bahari ya Hindi na njia zisizo rasmi mipakani, pamoja na ukwepaji kodi. Aidha, mapato yasiyo ya kodi yalivuka lengo kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki na kuimarika kwa usimamizi na ufuatiliaji wa vyanzo vya mapato husika.

13.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, fedha za misaada na mikopo nafuu zilizopokelewa zilikuwa shilingi bilioni 2,083.4. Mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara iliyopatikana ni shilingi bilioni 1,144.8 na mikopo kutoka katika soko la ndani ni shilingi bilioni 3,950.7.

14.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya shilingi bilioni 27,049.2, ambapo matumizi ya kawaida yalikuwa shilingi bilioni 19,099.9 na matumizi ya maendeleo yalikuwa shilingi bilioni 7,949.3. Vile vile, Serikali ililipa shilingi bilioni 6,659.6 kwa ajili ya mishahara ya watumishi na shilingi bilioni 599.94 kwa ajili ya madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi wa Serikali.   Kadhalika, katika kipindi hicho, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 7,701.7 kwa ajili ya kulipia kwa wakati mitaji (principal) na riba kwa mikopo ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

15.         Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2018/19 yanapatikana katika Sehemu ya Kwanza ya kitabu cha Mwongozo (Sura ya Pili).

Utekelezaji wa Baadhi ya Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2018/19 na Robo ya Kwanza ya Mwaka 2019/20

16.         Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2018/19 na robo ya kwanza ya mwaka 2019/20 ni pamoja na:
(i)           Mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere: Serikali iliendelea na utekelezaji wa mradi huu ambapo kazi zilizokamilika ni pamoja na: ujenzi wa daraja la muda namba 2; utafiti wa miamba na udongo; uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini (adit tunnel)wenye urefu wa mita 147.6 kuelekea kwenye mtaro wa chini kwa chini wa kuchepua maji ya mto Rufiji (diversion tunnel); na mtambo wa kuchakata kokoto (Batching Plant and Crusher) namba moja.
(ii)          Mradi wa Reli ya Kati ya Standard Gauge: Ujenzi wa reli ya kati ya Standard Gauge kwa sehemu Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 63 na sehemu ya Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 16.

(iii)        Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: ndege nne zimepokelewa ambapo mbili ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na mbili ni aina ya Airbus A220-300; kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege moja aina ya Bombadier Dash 8 Q400 inayotarajiwa kuwasili Desemba 2019; kusainiwa kwa mikataba na kulipa malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu ambapo mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya Bombardier Q400. Aidha, Shirika limeongeza idadi ya vituo vya safari za ndani kufikia 11 na nje ya nchi kufikia vituo sita.

(iv)        Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanga): Tanzania iliendelea na majadiliano ili kufikia makubaliano na Serikali ya Uganda na Mwekezaji (Host Government Agreement - HGA); tafiti za Mateocean, kijiolojia na kijiofizikia katika eneo la Chongoleani-Tanga zilikamilishwa; na kazi ya usanifu wa kina wa kihandisi (Detailed Engineering Design) wa eneo la ujenzi wa mradi inaendelea.
(v)          Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia – Lindi: Serikali inaendelea na majadiliano na kampuni za mafuta (Equinor na Shell) katika kitalu namba 1, 2, na 4 katika bahari kuu. Aidha,  tathmini ya Athari za Mazingira na Jamii  pamoja na Mpango wa Uhamishaji wa Wananchi watakaopisha eneo la mradi vimekamilika.
(vi)        Makaa ya Mawe Mchuchuma na Vanadium, Titaniumna Chuma Liganga: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilika kwa utafiti wa kina kuhusu wingi, aina na thamani za madini katika miamba ya Liganga na uhakiki wa mali za wananchi watakaopisha eneo la miradi.
(vii)       Shamba la Miwa na Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi: Hatua iliyofikiwa kwa upande wa Shamba la Mkulazi I, ni kukamilika kwa michoro ya ujenzi wa bwawa la maji lenye ukubwa wa mita za ujazo milioni 15 na maandalizi ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha sukari. Kwa upande wa Shamba la Mbigiri – Mkulazi II, hatua iliyofikiwa ni: kuendelea kwa ujenzi wa majengo ya kiwanda cha sukari; kuboresha miundombinu ya barabara na majengo; na kupatikana kwa mzabuni wa kutengeneza na kufunga mitambo ya kiwanda ambapo mkataba umesainiwa.
(viii)      Miradi ya Umeme: Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 Makambako – Songea umekamilika; na utekelezaji wa miradi ya kufua umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya nishati vikiwemo maji na gesi unaendelea. Aidha, Serikali imeendelea na juhudi za kupeleka umeme vijijini hususan kupitia awamu ya tatu ya miradi ya nishati vijijini (REA) ambapo hadi Septemba 2019, jumla ya vijiji 8,102 vilikuwa vimefikishiwa umeme kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara, sawa na asilimia 66.04.
(ix)        Miradi ya maji mijini na vijijini: Serikali iliendelea na utekelezaji wa miradi ya Maji ya Kitaifa kwa kukamilisha ulazaji wa mabomba, upanuzi na ukarabati katika maeneo yanayohudumiwa na miradi; na kuboresha huduma za maji vijijini ambapo miradi 1,659 ya maji vijijini imekamilika. Aidha,  miradi 653 ya maji vijijini ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
(x)          Miradi ya Viwanda: Serikali inaendelea kuimarisha Shirika la Viwanda Vidogo - SIDO; ukarabati na upanuzi wa kiwanda cha ngozi na bidhaa za ngozi cha Karanga - Moshi; na kuimarisha Shirika la Nyumbu ili kuongeza uzalishaji ikiwemo kuzalisha magari ya zimamoto.
(xi)        Barabara na Madaraja: Serikali imeendelea kugharamia ujenzi wa barabara za lami nchini ambapo mtandao wa barabara kuu umefikia kilomita 8,306 na mtandao wa barabara za mikoa umefikia kilomita 1,756; ujenzi wa madaraja yafuatayo umekamilika: Sibiti (Singida), Momba (mpakani mwa Songwe na Rukwa), Mlalakuwa (Dar es Salaam), na Lukuledi (Lindi). Aidha, ujenzi wa barabara na madaraja mengine upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
(xii)       Meli katika Maziwa Makuu: ujenzi wa meli ya MV Mbeya katika Ziwa Nyasa umekamilika. Vilevile, mikataba ya ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli katika Ziwa Victoria na Tanganyika imeandaliwa.

(xiii)      Viwanja vya Ndege: Ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria (Terminal III) la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere umekamilika na jengo hilo kuanza kutumika. Ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Mwanza umefikia asilimia 95. Aidha, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege katika baadhi ya mikoa upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
(xiv)      Bandari: uboreshaji wa gati Na.1 na Na. 2 katika bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa gati la RoRo vimekamilika. Aidha, uboreshaji wa gati Na. 3 umefikia asilimia 60 na uboreshaji wa bandari za Tanga na Mtwara unaendelea.
(xv)       Uwekezaji wa Sekta Binafsi: Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kufutwa na kupunguzwa kwa ada na tozo 54 ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanya biashara na wawekezaji na kuzinduliwa na kuanza uzalishaji katika viwanda saba (7) ambavyo ni kiwanda cha Pipe Industries Co. Limited, kiwanda cha Chai cha Kabambe (Njombe), kiwanda cha Yalin Cashewnut Company Ltd (Mikindani – Mtwara), kiwanda cha 21st Century Food and Packaging,kiwanda cha kusaga mahindi cha Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited(MeTL), kiwanda cha bidhaa za plastiki cha Plasco Pipelines Co Ltd,  kiwanda cha kufungasha na kuhifadhi parachichi (Rungwe Avocado) na kiwanda cha kuchakata parachichi kwa ajili ya kutengeneza mafuta (KUZA Afrika).

17.         Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2018/19 na robo ya kwanza ya mwaka 2019/20 yameelezwa kwa kina katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Tatu).

C.           MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA MITANO KWA KIPINDI CHA 2016/17 HADI ROBO YA KWANZA YA  2019/20

18.         Mheshimiwa Spika, yapo mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/17 hadi Septemba 2019. Mafanikio hayo ni pamoja na:

   (i)        Ukuaji wa Uchumi: Kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Taifa, ambapo uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 7.0 mwaka 2018 kutoka ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2017 na mfumuko wa bei kuendelea kupungua na kufikia asilimia 3.4 Septemba 2019.
  (ii)        Ukusanyaji wa Mapato: Kuongezeka kwa mapato ya ndani kutoka wastani wa shilingi bilioni 800 kwa mwezi katika mwaka 2016/17 hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 1,292.6 kwa mwezi katika mwaka 2018/19 kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika ukusanyaji wa mapato. Aidha, juhudi hizo zimeendelea kuleta mafanikio ambapo mapato ya ndani kwa mwezi Septemba 2019 yamefikia shilingi bilioni 1,740.2.

(iii)        Ulipaji wa Deni la Serikali: Tangu mwaka 2016/17 hadi Septemba 2019 Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 24,499.2 kwa ajili ya deni lililoiva la fedha zilizokopwa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
(iv)        Ulipaji wa Mishahara: Mishahara ya watumishi wa Serikali yenye jumla ya shilingi bilioni 22,169.9 ililipwa kwa wakati katika kipindi chote cha 2016/17 hadi Septemba 2019.
  (v)        Barabara na Madaraja: Ujenzi wa barabara 23 za lami umekamilika na hivyo kuongeza mtandao wa barabara kuu za lami kutoka kilomita 7,646 Juni 2016 hadi kilomita 8,306 Juni 2018 na mtandao wa barabara za mikoa umeongezeka kutoka kilomita 1,398 hadi kilomita 1,756; Barabara ya juu ya Mfugale (TAZARA – Dar es Salaam), ilikamilika na kuanza kutumika; ujenzi wa barabara unganishi ya juu ya Ubungo Interchange (Dar es Salaam), unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 55; Madaraja yaliyokamilika ni pamoja na daraja la Magufuli katika Mto Kilombero (Morogoro), Kavuu (Katavi), Sibiti (Singida), Momba (mpakani mwa Songwe na Rukwa), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Lukuledi (Lindi) na daraja la Waenda kwa Miguu la Furahisha (Mwanza) na kuanza kwa ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza). Aidha, ujenzi wa barabara na madaraja mengine upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
(vi)        Reli: Ujenzi wa reli ya kati ya Standard Gauge unaendelea ambapo sehemu ya Dar es Salaam – Morogoro (km 300) ujenzi umefikia asilimia 63 na Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 16. Aidha, ukarabati wa reli ya kati ya zamani, madaraja, na ujenzi wa makalavati upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Pia, ukarabati wa kipande cha reli ya Tanga – Moshi (km 353) umekamilika na kuanza kufanya kazi.
(vii)        Nishati: Uwezo wa kuzalisha umeme katika Gridi ya Taifa umeongezeka kufikia megawati 1,613.52; Idadi ya vijiji vilivyounganishiwa umeme imefikia 8,102 kati ya Vijiji 12,268 vya Tanzania Bara sawa na asilimia 66.04; na utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere utakaozalisha MW 2,115 unaendelea.
(viii)        Shirika la Ndege Tanzania: Jumla ya ndege mpya 11 zimenunuliwa ambapo ndege saba zimepokelewa. Utengenezaji wa ndege moja upo katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuwasili nchini kabla ya mwisho wa mwaka 2019. Vilevile, ndege 3 zimeanza kutengenezwa baada ya malipo ya awali kulipwa. Aidha, uboreshaji wa Shirika la Ndege la Tanzania umeongeza huduma za usafiri wa anga kufikia vituo 11 nchini na vituo 6 nje ya nchi.
(ix)        Viwanja vya Ndege: Jengo la Tatu la Abiria (Terminal III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere limekamilika na kuanza kutumika; awamu ya kwanza ya ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro umekamilika; ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza umekamilika kwa asilimia 95; na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya mikoa unaendelea na umefikia hatua mbalimbali za utekelezaji.
  (x)        Bandari: Upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam unaendelea ambapo gati Na.1 na Na. 2 na ujenzi wa gati la Ro-Ro umekamilika na kuwezesha meli ya kwanza yenye uwezo wa kubeba magari 6,000 kuhudumiwa katika gati hilo tarehe 15 Septemba, 2019. Uboreshaji wa gati Na. 3 umefikia asilimia 60. Aidha, uboreshaji wa bandari za Tanga, Mtwara na bandari za maziwa makuu unaendelea.
(xi)        Usafiri katika Maziwa Makuu: Ujenzi wa matishari mawili (2) na meli ya MV Mbeya katika Ziwa Nyasa umekamilika; ujenzi na ukarabati wa meli tano (5) katika Ziwa Victoria (ikiwemo MV Victoria, MV  Butiama, MV Umoja na MV Serengeti) unaendelea; na mikataba ya ujenzi wa meli moja (1) mpya na ukarabati wa MV Liemba katika Ziwa Tanganyika imeandaliwa.
(xii)        Kilimo: uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2018/19 ulifikia tani 16,408,309 na hivyo kuwa na ziada ya tani 2,565,774 za mazao ya chakula. Hivyo, kiwango cha Utoshelevu wa Chakula kilikuwa asilimia 119.
(xiii)        Madini: Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya kuboresha mazingira ya biashara kwenye sekta ya madini ikihusisha vituo vya umahiri (centres of excellence) katika mikoa saba, vituo vitatu vya mfano, Jengo la Taaluma ya Madini katika Chuo cha Madini, Kituo cha Pamoja cha Biashara ya Madini (One Stop Centre) Mirerani, Jengo la Wafanyabiashara (Brokers House) Mirerani, uanzishwaji wa masoko 28 ya madini na vituo vidogo 11 vya ununuzi wa madini katika mikoa 24 nchini, uwekaji wa mfumo wa ulinzi wa kidigitali Mirerani, ununuzi wa mtambo wa uchorongaji miamba kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo na kufutwa kwa kampuni ya Madini ya ACACIA na kuundwa kampuni mpya ya Twiga Mineral Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania (hisa asimilia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84).
(xiv)        Viwanda: Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo jumla ya viwanda 3,530 vimejengwa katika mikoa mbalimbali.
(xv)        Huduma za Afya: Mafanikio yaliyopatikana yanajumuisha kuendelea na ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa, kanda na kitaifa; ujenzi wa Hospitali mpya za Wilaya 67 na pia kuanza maandalizi ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru (Dodoma), Hospitali ya Wilaya ya Tunduma (Songwe) na Hospitali ya Manispaa ya Ubungo (Dar es Salaam); ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za Afya (470) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98; kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa nyumba 301 za watumishi wa afya; na kuendelea na ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
(xvi)        Huduma za Maji: Mradi wa kuboresha huduma za maji Dar es Salaam (utekelezaji umefikia wastani wa asilimia 74); Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria: ulazaji wa bomba la kusambazia maji katika miji ya Isaka, Tinde na Kagongwa imekamilika kwa asilimia 99; na ujenzi wa miundombinu ya maji katika miji ya Tabora, Igunga, Uyui na Nzega pamoja na vijiji 89 vilivyo pembezoni mwa bomba kuu umefikia asilimia 78; Miradi 1,659 ya maji vijijini imekamilika na ujenzi na ukarabati wa miradi 653 ya maji vijijini ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

(xvii)        Elimu: Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kugharamia elimumsingi bila ada; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote; Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikamilika na kuzinduliwa; utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu umeendelea pamoja na uimarishaji wa vyuo vya ufundi stadi (VETA).
(xviii)        Kuhamishia Shughuli za Serikali Makao Makuu Dodoma: Serikali ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imefanikisha ndoto ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere kuhamishia Makao Makuu ya Serikali jijini Dodoma kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi ambapo jumla ya watumishi 8,883 wa Wizara na Taasisi za Serikali  wamehamishiwa Makao Makuu ya Serikali, Dodoma na ujenzi wa ofisi 23 za Wizara katika mji wa Serikali, Mtumba umekamilika, ikijumuisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

19.         Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti yanapatikana katika  Sehemu ya Kwanza -  Sura ya Pili ya Kitabu cha Mwongozo na Kitabu cha Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2016/17 hadi robo ya kwanza ya Mwaka 2019/20.

D.           CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI NA HATUA ZA KUKABILIANA NAZO

20.         Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2018/19 ilikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuwepo kwa mahitaji makubwa yasiyowiana na uwezo wa mapato; ukwepaji kodi kwa njia mbalimbali ikiwemo kutokutoa stakabadhi za kielektroniki na kuendesha biashara za magendo hususan kupitia bandari bubu na  katika maeneo ya mipakani; mabadiliko ya viwango vya riba katika masoko ya fedha ya nje; kutopatikana kwa misaada na mikopo kutokana na baadhi ya Washirika wa Maendeleo kutotimiza ahadi zao kwa wakati; na ukosefu wa takwimu za uwekezaji wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

21.         Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa bajeti, Serikali itaendelea kuchukua hatua zifuatazo: kuendelea kuwianisha mapato na matumizi; kuimarisha ulipaji wa kodi wa hiari kwa kutekeleza Mpango wa Kusimamia Vihatarishi vya Mwitikio wa Ulipaji Kodi; kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi ya mashine za stakabadhi za kielektroniki kupitia matumizi ya Mfumo ulioboreshwa; kuongeza doria na ukaguzi unaolenga kudhibiti biashara za magendo; kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji; kukuza soko la fedha la ndani; kuendeleza majadiliano na Washirika wa Maendeleo na taasisi za fedha za nje; kutekeleza mwongozo wa ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo; na kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kupata taarifa za uwekezaji wa sekta hiyo katika uchumi.


E.           MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2020/21

22.         Mheshimiwa Spika, misingi iliyozingatiwa katika kuweka malengo ya uchumi jumla ni pamoja na: Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, utulivu na umoja hapa nchini na katika nchi jirani; kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya fedha ya ndani na ya kimataifa; na kuwepo kwa hali nzuri ya hewa itakayowezesha uzalishaji wa chakula cha kutosha.

23.         Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya uchumi jumla yatakayozingatiwa katika muda wa kati ni pamoja na:-
(ii)          Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 - 5.0;
(iii)         Mapato ya ndani kufikia asilimia 14.8 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 na kufikia wastani wa asilimia 14.9 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2022/23;
(iv)         Matumizi ya Serikali kuwa asilimia 21.7 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 na asilimia 20.9 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23;
(v)          Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) inakuwa chini ya asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
(vi)         Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4.0).


Mfumo wa Awali wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2020/21

24.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Mapato ya ndani (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadiriwa kuongezeka hadi shilingi bilioni 23,456.3 mwaka 2020/21 kutoka makadirio ya shilingi bilioni 23,045.3 mwaka 2019/20 na kukadiriwa kuongezeka kwa wastani wa asilimia 8.8 katika muda wa kati. Uwiano wa mapato ya ndani kwa mapato yote unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 68.3 ya bajeti ya mwaka 2020/21 hadi asilimia 73.7 mwaka 2022/23. Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 4.3 hadi shilingi bilioni 19,761.2 mwaka 2020/21 kutoka shilingi bilioni 18,955.2 mwaka 2019/20 na kukua kwa wastani wa asilimia 8.9 katika muda wa kati. Mapato yasiyo ya kodi (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadariwa kuwa shilingi bilioni 3,601.3 mwaka 2020/21 na kuongezeka kufikia shilingi bilioni 4,340.0 mwaka 2022/23.

25.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21 jumla ya misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,268.6 ambapo Misaada ya Kibajeti (General Budget Support- GBS) inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 154.2, Misaada ya Mifuko ya Pamoja ya Kisekta (Basket Funds)shilingi bilioni 172.9 na Misaada ya Miradi (Project Funds) shilingi bilioni 941.5. Aidha, nakisi ya bajeti inayojumuisha misaada inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 3,943.4 sawa na asilimia 2.5 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2020/21 ambapo jumla ya shilingi bilioni 2,355.3 zitagharamiwa na mikopo ya nje na shilingi bilioni 1,588.2 zitagharamiwa na mikopo ya ndani sawa na asilimia 1 ya Pato la Taifa.

26.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21 matumizi ya Serikali yanakadiriwa kuongezeka hadi shilingi bilioni  34,360.2 sawa na asilimia 21.7 ya Pato la Taifa kutoka shilingi bilioni 33,105.4 mwaka 2019/20. Matumizi ya kawaida yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 4.7 hadi shilingi bilioni 21,660.7 sawa na asilimia 13.7 ya Pato la Taifa na matumizi ya maendeleo yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni  12,699.4 sawa na asilimia 8.0 ya Pato la Taifa.

27.         Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu sera za mapato na matumizi katika muda wa kati yapo katika Sehemu ya Kwanza – Sura ya Tatu ya Kitabu cha Mwongozo.

F.            MAELEKEZO MAHSUSI YA MWONGOZO

28.         Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21 umeainisha maelekezo mbalimbali ambayo Maafisa Masuuli watatakiwa kuyazingatia wakati wa uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa. Hivyo, Maafisa Masuuli watatakiwa kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo na kusimamia Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake. Aidha, Kamati za Mipango na Bajeti za kila Fungu zitatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni ya 17(3) ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za mwaka 2015. Baadhi ya maelekezo yanayotakiwa kuzingatiwa na Maafisa Masuuli ni:
(i)           Kufanya mapitio ya utekelezaji wa bajeti na kubuni mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye Mafungu;
(ii)          Kubuni na kuboresha mifumo ya usimamizi wa mapato ikiwemo kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari;
(iii)        Kupitia, kurekebisha na kuandaa sheria ndogo ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato na utawala bora katika Mamlaka za Serikali za Mitaa;
(iv)        Kuhakikisha gharama za miradi inayoendelea zinajumuishwa kwenye mpango wa muda wa kati na bajeti kabla ya kuanzisha miradi mipya;
(v)          Kufanya ukadiriaji sahihi wa stahili za kisheria kama vile posho, pango, umeme, simu na maji kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia mabadiliko baada ya shughuli za Serikali kuhamishiwa Dodoma;
(vi)        Kuweka kipaumbele katika utengaji wa fedha za kulipia madeni yaliyohakikiwa kwa kutumia ukomo wa bajeti uliotolewa;
(vii)       Kuhakikisha Kamati za Bajeti za Mafungu zinafanya kazi kwa kuzingatia Kifungu cha 18(2) cha Sheria ya Bajeti, Sura 439 na Kanuni zake;

(viii)      Kuandaa ikama na makadirio ya bajeti ya mishahara kwa mwaka 2020/21 kwa kuzingatia Waraka wa Katibu Mkuu UTUMISHI;
(ix)        Kuandaa na kuwasilisha mikakati ya uwekezaji, mwongozo wa gawio na mipango ya biashara kwa Msajili wa Hazina kwa ajili ya kuidhinishwa;
(x)          Kuandaa na kuwasilisha kwa Msajili wa Hazina mpango mkakati wa kuboresha utendaji wa mashirika ili kuepuka kujiendesha kwa hasara;
(xi)        Kubuni mikakati ya kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani;
(xii)       Kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 10(A) cha Sheria ya Fedha ya mwaka 2015 kwa kutenga na kuwasilisha kwa wakati katika Mfuko Mkuu wa Hazina michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi;
(xiii)      Kuzingatia viwango vya ukomo wa bajeti vilivyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango; na
(xiv)      Kuandaa mpango na bajeti kwa kuzingatia muundo wa Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) na kuwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uchambuzi. Mawasilisho hayo yanatakiwa kufanyika wiki ya tatu ya Januari, 2020 baada ya kuidhinishwa katika ngazi za maamuzi husika ikijumuisha Mabaraza ya Wafanyakazi kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma, Sura 105.

29.         Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu maelekezo mahsusi ya Mwongozo yanayotakiwa kuzingatiwa na Maafisa Masuuli yanapatikana katika Sehemu ya Pili ya Kitabu cha Mwongozo (Sura ya Kwanza na Sura ya Pili).

G.           MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21

30.         Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21 yameandaliwa kwa kuzingatia maeneo manne ya kipaumbele yanayojumuisha miradi ya kielelezo iliyobainishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Maeneo ya kipaumbele pamoja na baadhi ya miradi itakayopewa kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo:

(i)           Ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda
Kuendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuboresha upatikanaji wa mbegu na pembejeo za kilimo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji, maghala na masoko; kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini, hususan za kilimo; kuimarisha Shirika la Viwanda Vidogo – SIDO kuweza kuhudumia wananchi wengi zaidi ili kuchochea mageuzi ya viwanda nchini; kuanzisha na kuendeleza maeneo ya viwanda (Industrial parks) na Kanda Maalum za Kiuchumi; kuboresha utendaji kazi na kutumia taasisi za umma za utafiti na huduma za viwanda; kuanza shughuli za ujenzi katika mradi wa Umeme wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na Kiwanda cha Kufua Chuma cha Liganga; na kuendeleza Shamba la Miwa na kuendelea na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi.
(ii)          Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu
Serikali itaendelea: kuimarisha upatikanaji wa elimu na huduma za ustawi wa jamii; kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza upatikanaji  wa dawa muhimu na vifaa tiba kwa ajili ya kutoa huduma za tiba kwa wananchi; kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama vijijini na mijini; kuimarisha usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi; kuimarisha shughuli za utawala bora ikiwemo Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; kuendelea kutekeleza sera ya elimumsingi bila ada, kusomesha wataalam na mafundi wengi wenye fani na ujuzi maalum; na kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

(iii)        Ujenzi wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji wa Biashara na Uwekezaji:
Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu, ikijumuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji (reli, madaraja, barabara na bandari), usafiri wa anga na usafiri wa majini (magati, meli na vivuko); kuendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia uwekezaji ikiwemo kutekeleza Blue Print; na kuimarisha mfumo wa ugawaji na usimamizi wa ardhi. Miradi itakayopewa msukumo ni: Mradi wa kufua umeme wa Maji wa Julius Nyerere - MW 2,115; ujenzi wa reli ya kati ya Standard Gauge; kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania).

(iv)        Kuimarisha Usimamizi na Utekelezaji wa Mpango
Katika mwaka 2020/21, utekelezaji  Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) unatarajiwa kukamilika ambapo Serikali itaandaa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Miaka Mitano.

Miradi ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi

31.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira wezeshi ili kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi au kwa utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika maeneo ya kipaumbele. Baadhi ya miradi itakayotekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni pamoja na: Mradi wa uzalishaji wa Dawa Muhimu na Vifaa Tiba; Kusambaza Gesi Asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara; ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne na Kituo cha Kibiashara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; Ujenzi wa Reli ya standard gauge ya Mtwara – Mbamba Bay na matawi ya Mchuchuma na Liganga; Ujenzi wa Hosteli za wanafunzi katika Chuo cha Elimu ya Biashara (kampasi ya Dar es Salaam na Kampasi ya Dodoma) na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP - Dodoma); Uendeshaji wa Huduma ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam Awamu ya Kwanza; na Ujenzi wa Reli ya standard gauge ya Tanga - Arusha – Musoma pamoja na matawi ya Engaruka na Minjingu.
32.         Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Maeneo ya Kipaumbele kwa mwaka 2020/21 yapo katika Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Nne).


H.           HITIMISHO

33.         Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali, napenda kuahidi kuwa maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango yatazingatiwa kikamilifu katika uandaaji wa  Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Aidha, Mapendekezo haya yatazingatiwa na Maafisa Masuuli wote wakati wa kuandaa Mipango na Bajeti za Mafungu yao. Kutokana na Mapendekezo ya Mpango huu, Serikali itaainisha na kuandaa mipango ya kisekta, kitaasisi na kimaeneo ambayo tunaamini kuwa utekelezaji wake utachochea ujenzi wa uchumi wa viwanda, mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu. Hivyo, Maafisa Masuuli wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi na Mashirika ya Umma wanaelekezwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango na ushauri makini wa Bunge wakati wa kuandaa Mipango na Bajeti za Mafungu yao kwa Mwaka 2020/21. Vile vile, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kuzingatia kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21 na kusimamia Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake.

34.         Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napenda kupongeza kwa dhati hatua zilizochukuliwa na Ofisi ya Bunge chini ya uongozi wako kupunguza matumizi kwa kuanza kutekeleza mfumo wa Bunge Mtandao (e-parliament) na kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kuchapisha nyaraka mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Waheshimiwa Wabunge.  Natoa rai kwa Wizara na Taasisi zote za Umma kufuata mfano huu mzuri.

35.         Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kuishauri Serikali kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21.

36.         Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527