MWAITEBELE : VIONGOZI WA UMMA MSIFANYE UBAGUZI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA KWA WANANCHI

Na Salvatory  Ntandu 
Imebainika kuwa kukiukwa kwa nguzo saba za maadili kwa baadhi ya viongozi wa Umma katika maeneo yao ya kazi husababisha wananchi kukata tamaa hali ambayo imetajwa kurudisha nyuma maendeleo.

Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Mkuu wa Kanda,Ofisi ya Rais Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi (Tabora) Gerald Mwaitebele wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha ziara ya siku mbili ya kutembelea vituo vya redio mjini Kahama.

Amesema baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa wakikiuka nguzo saba za maadili ambazo ni uadilifu,uaminifu,uwazi,ushirikishwaji,uzalendo,uwajibikaji na ufanisi katika vituo vyao vya kazi na kusababisha kutoa maamuzi ambayo wakati mwingine huwa na athari kwa wananchi.

“Sisi tumeamua kuwakumbusha viongozi wote wa Umma nguzo hizi za maadili kupitia vyombo vya habari vilivyopo katika wilaya ya Kahama ili pengine kwa namna mmoja au nyingine kama wamesahau waweze kukumbuka wajibu wao”,alisema Mwaitebele.

Amefafanua kuwa endapo maadili hayo yatazingatiwa kwa usahihi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa itasaidia kupunguza malalamiko kwa wananchi wanyonge ambao wamekuwa wakikosa haki zao na kutokuwa na imani nao.

Katika hatua nyingine Mwaitebele amewataka wananchi kuwafichua vitendo vya ukiukwaji wa maadili vinavyofanywa na viongozi wa umma katika jamii zao,kuchagua viongozi waadilifu na wasio toa rushwa.

“Katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa chagueni viongozi waadilifu msichague wabadhilifu ambao wakiingia madarakani wataleta migogoro katika jamii zenu na kurudisha nyuma shughuli za maendeleo”,alisema Mwaitebele.

Katika ziara hiyo ya kutembelea vituo vya Redio vya Mjini Kahama Ofisi ya Rais sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya magharibi (TABORA) imetembelea vituo vitatu vya redio ambavyo ni Divine FM,Huheso FM na Kahama FM.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post