KITABU CHA MKAPA, RAIS MAGUFULI ALIKISOMA KABLA HAKIJAANDIKWA

Na: Lillian Shirima – Habari MAELEZO

Novemba 12, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania,Dkt. John Magufuli alizindua kitabu cha maisha binafsi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa cha (My Life My Purpose) (Maisha Yangu, Kusudi Langu) , hafla hiyo  iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa viongozi wengi wakiwemo na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.

Kitabu hicho chenye kurasa 316, na sura 16 zilizogawanywa kwenye sehemu kuu tatu, kimesheheni wingi wa nasaha na ushauri lakini pia kinatoa mafundisho mengi kwa viongozi wa baadaye jambo ambalo Rais John Pombe Magufuli aliliona mapema pengine kabla ya kuandikwa kwenye kitabu hicho.

Katika sehemu ya mwisho ya kitabu inayoeleza kwa ufupi maisha ya Mzee Mkapa baada ya kumaliza miaka kumi ya kulitumikia taifa kwa ngazi ya urais, Mkapa anatoa ushauri kwa kutaja mambo sita ambayo kiongozi anawajibu kwa kuyazingatia.

Mambo hayo ni kuonyesha nia na bidii kwa majukumu unayopewa na wananchi, kuwa tayari kuwashirikisha wengine katika mawazo, mafanikio, matatizo na upimaji wa utekelezaji, kutofanya kazi kwa kukurupuka na kutotabirika.

Mengine ni kufuata  na kutii sheria na taratibu, kuwa tayari kusikiliza na mwisho kutafuta mlezi (mentor) kama ambavyo yeye mwenyewe Mzee Mkapa anavyoeleza mlezi wake kuwa alikuwa Mwalimu Julius Nyerere.

Katika mahojiano yaliyofanyika na mtaalam wa masuala ya siasa Bwana Severine Kapinga kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salam, (UDSM), anasema, ushauri aliotoa Mzee Mkapa kuhusu wajibu wa kiongozi na mambo anayotakiwa kuzingatia hapana shaka Rais John Magufuli alianza kuyaishi na kuyazingatia kabla kitabu cha Mkapa hakijaandikwa 2016.

Anaongeza kuwa, nchi yoyote duniani toka ilipopata uhuru ikipita miaka 50 ni lazima nchi hiyo ifikie wakati wa kuweza kujipambanua na kujielewa ipo wapi, inataka kufika wapi na imekwama wapi; kazi ambayo sio ya sera pekee bali ni kazi itakayofanywa na kiongozi mwenye nia ya kuwatumikia wananchi kwa dhati.

“Hii sio kazi ya kisera tu, ni kazi ambayo itaongozwa na kiongozi ambaye amechaguliwa na watu na yeye sasa ndiye anayetakiwa kubeba maono ya watu na dhamira ya walio wengi’. Anasema Bw. Kapinga.

Rais Magufuli amethubutu katika hili kuonesha nia na bidii ya kazi katika majukumu aliyopewa na wananchi na kwamba ameweza kuvaa taswira ya maono ya wananchi kwa namna anavyoisimamia na kuiongoza nchi, uwajibikaji wake umekuwa chachu kwa wananchi kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, anasema mageuzi makubwa yanayoonekana sasa yanatokana na uwajibikaji wa Rais Magufuli katika kusimamia rasilimali za nchi, nidhamu kwenye matumizi ya fedha za umma na maarifa katika kushughulikia matatizo ya wananchi wanyonge.

Mara kadhaa tunashuhudia Rais Magufuli akifanya mikutano na watendaji wa Serikali kuanzia Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya na Makatibu Watendaji wa Tarafa. Mathalani, Septemba 2,mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na Maofisa Watendaji wa Kata kutoka nchi nzima Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mbali na kuwashirikisha katika maamuzi kama ambavyo Mzee Mkapa ameshauri katika kitabu chake, Rais Magufuli ameenda mbali zaidi na kuwaasa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kata wanazozisimamia zinakuwa na ulinzi na usalama.

Rais Magufuli aliwaambia, “hakuna shughuli za maendeleo zinazoweza kufanyika bila kuwa na amani, ni lazima wananchi wafanye kazi bila hofu , bila bugudha…”.

Ushauri wa Mzee Mkapa kwa viongozi wajao ni dhahiri ulianza kutekelezwa kitambo.

Kundi lingine lililokutana na Rais Magufuli Juni,mwaka huu ni wafanyabiashara kutoka katika wilaya zote nchini kwa nia ya kutaka kujadiliana kwa uwazi namna ya kutatua changamoto walizonazo na kubuni njia bora za kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Wengine ni Mabalozi wetu wanaotuwakilisha katika nchi mbalimbali, wachimbaji madini na wadau wa sekta ya madini, na hata wachezaji wa timu ya Taifa, (Taifa Star) Hakika Rais hafanyi kazi kwa kukurupuka au kutotabirika isipokuwa kushirikisha kada tofauti katika mipango ya maendeleo, Ushauri aliotoa Mzee Mkapa katika kitabu chake.

Mara kadhaa Rais Magufuli amesikika akisema yeye si wa kundi lile, yeye ni wa wanyonge na kwamba Watanzania wanyonge ndio watakajenga nchi hii.

Kwa kauli hii Bwana Kapinga anasema, Rais Magufuli angekuwa upande wa watu wachache miradi mikubwa tunayoiona sasa isingekuwepo lakini kwa kuwa ameamua kusimama upande wa Watanzania wanyonge mwamko wa watu kujituma kufanya kazi umekuwa mkubwa.

Wakati wa uzinduzi wa Kitabu hicho,Rais Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi alimshukuru Mzee Mkapa kwani katika uongozi wake wa Awamu ya Tatu mambo mengi yamefanyika ikiwa ni pamoja na kujenga barabara kwa fedha za ndani.

Alieleza namna alivyovutiwa na sura nyingi za Kitabu hicho ambazo zimeeleza jinsi ya kujitegemea, jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na kusisitizwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Akitoa mfano mdogo wa hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imeleta mwamko wa watu, Bwana Kapinga amesema, kuanzishwa kwa mpango wa utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo wenye biashara chini ya mzunguko wa shilingi milioni 3 kwa kiasi kikubwa umewaweka wajasiriamali katika mazingira huru yakujitegemea.

Mara baada ya zoezi la ugawaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara ndogondogo kukamilika, wengi wao wameanza kutambua kuwa nchi ipo katika mageuzi ya kiuchumi na wanashiriki kuchangia maendeleo ya nchi.

Anasema, ukifika Kariakoo, Tazara na maeneo ya wafanyabiashara ndogondogo, wamachinga,wanaweza kukueleza juu ya miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa, madaraja na barabara za juu kwasababu wanatembea kwa amani wakifanya biashara pasipo chuki na Serikali.

“Siku hizi tumesahau mambo ya kukimbizana na wamachinga na mama ntilie mjini, kamatakamata ambayo haina mwelekeo haipo tena kwa sababu Rais aliamua kutafuta majibu ya kero za wafanyabiashara ndogondogo kwa kuwapa vitambulisho na ruhusa kufanya shughuli zao bila bughudha”, anasema Kapinga.

Tunamwona Rais akifanya ziara za ndani zaidi kuliko ziara za nje ya nchi kwa msingi wa kuwa tayari kusikiliza matatizo ya wananchi na kutafuta ufumbuzi wamatatizo hayo ikiwa ni pamoja na kuhakiki taarifa za maendeleo anazopewa na wasaidizi wake.

Hakuna ziara anayofanya bila kuwa na taarifa ya eneo husika hii ni kutokana na uzoefu wa muda mrefu katika kulitumikia taifa ndio unaopelekea kuwepo kwa ziara za kushtukiza.

Bwana Kapinga anasema, hatua hii ndio inayofanya wote waliokuwa wavivu wa kwenda kwa wananchi kutambua kuwa kazi kubwa ipo kwa wananchi na sio nje ya nchi na kwamba Awamu ya Tano imerudisha mamlaka kwa wananchi kwasababu viongozi wakuu wa Serikali wanakwenda kwa wananchi mara kwa mara.

“Huwezi kuwa na mamlaka na Serikali kama huioni, tunasema hii ndio Serikali ya watu…. viongozi wanathamini watu, Rais amekaa nafasi ya waliokosa, nafasi ya mwananchi mwenye hali ngumu, kwa sababu amepewa dhamana na wao, anaumia kama anavyoumia yule mwananchi wa mwisho”, anasema Bwana Kapinga.

Ni katika kitabu hicho Mzee Mkapa ameshauri viongozi kutafuta mlezi (mentor) na kwamba kwake yeye Mwalimu Nyerere alikuwa mezi wake. Sio siri Mzee Mkapa ndiye aliyemuibua Rais Magufuli katika medani za siasa. Ndiye aliyetambua uwezo wake wa kazi katika kusimamia maamuzi sahihi na kuyatekeleza kwa ufasaha, na Mzee Mkapa ndiye aliyekuwa tayari kumtia nguvu pale alipokutana na vikwazo katika utekelezaji wa majukumu ya kazi kwa maslahi ya taifa.

Ushauri wa mambo sita yaliyotajwa katika kitabu cha Mzee Mkapa “Maisha Yangu Kusudi Langu” tunaona kuwa,Rais John Pombe Magufuli ameutekeleza mapema na ndiyo maana tunasema , alikisoma kitabu kabla hakijaandikwa, alianza kuzingatia mengi kwa vitendo na hata katika hotuba yake za uzinduzi wa kitabu hiki amekiri kuwa Mzee Mkapa ndio shujaa wake, ametoa wito kwa Watanzania kuwaenzi na kuwatunza wazee wote wakiwemo viongozi wastaafu ambao ama kwa hakika tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post