TUNDU AINUSA TANZANIA... YUPO KENYA SASA

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki  Tundu Lissu yupo nchini Kenya, akisubiri ‘amri’ ya kuingia nchini endapo atahakikishiwa usalama wake.

Akizungumza na kituo cha Televisheni cha KTN nchini Kenya jana tarehe 28 Novemba 2019, Lissu amesema amepona lakini hali ya usalama wake bado si shwari.

“Bado kuna vitisho vya aina hii, lazima watu wenye busara wakae na kuangalia namna nzuri ya kufanya ili niweze kurudi nyumbani,” amesema Lissu.

Amemweleza mwandishi wa kituo hicho, kwamba kuna watu ambao wasingependa kuona akirudi na siku moja baadaye anapigwa risasi tena.

Lissu amesema “nafikiri hakuna mtu anayetaka kuona narudi nyumbani na keshokutwa ninapigwa risasi tena.”

Hata hivyo amesema, bado jitihada zinafanywa na ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha ataporejea kunakuwa na usalama wa kutosha.

Amesisitiza, hataki kuishi nje ya Tanzania kwa kuwa, alikwenda kwa ajili ya matibabu na sasa matibabu hayo yamekwisha

“Mimi sitaki kabisa kuishi uhamishoni. Nilienda kwenye matibabu nimeshatibiwa nasubiri niambiwe usalama wangu utakuwaje katika mazingira halisi,” amesema.

Lissu alishambiliwa kwa risasi tarehe 7 Septemba 2017, akiwa nyumbani kwake eneo la ‘Area D’ jijini Dodoma na kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa huo.

Baadaye alihamishiwa Nairobi nchini Kenya ambapo tarehe 6 Januari 2018 alipelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambapo yupo mpaka sasa.

Shambulizi dhidi ya Lissu, lilitokea muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkutano wa Bunge wa asubuhi.
Chanzo - MwanahalisiOnline

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527