RAIS MAGUFULI: “TUNAZO FEDHA ZA KUKAMILISHA HOSPITALI YA UHURU”

Na Englibert Kayombo, WAMJW – Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inayo fedha za kutosha kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Uhuru. 


Rais Magufuli amesema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa wilayani Chamwino, Dodoma. 

“Fedha ya ujenzi wa hospitali ipo, tunayo Billioni 3.4” amesema Rais Magufuli ambaye ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

Rais Magufuli amesema kuwa mwanzoni TBA ilipewa kazi ya ujenzi wa hospitali hiyo lakini hawakusimamia vizuri ujenzi kupelea Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo kuchukua maamuzi ya kukabidhi kazi kwa Jeshi la Kujenga Taifa ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.

Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia Jenarali Charles Mbuge aliyepewa jukumu la kusimamia ujenzi wa Hospitali hiyo amesema kuwa Jeshi lake linauwezo wa kufanya kazi hiyo na kuikamilisha ndani ya muda uliopangwa.

“Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, Jeshi letu lina nguvu ya kutosha na tutamaliza kwa muda kazi hii, sina mipango mingine ni kumaliza tuu” amesema Brigedia Jenerali Mbuge.

Mnamo tarehe 9 Desemba, 2018, Rais Magufuli alitoa maagizo ya fedha zilizotengwa kugharamia sherehe za uhuru kiasi cha Shilingi Milioni 995 kutumika kujenga hospitali katika Mkoa wa Dodoma. Kukamilika kwa hopitali hiyo kutatatua kero waliyokuwa wanaipata wananchi ya umbali wa kufuata huduma za afya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527