KAMPUNI YA NYANZA YAPIGWA MARUFUKU DAR


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda ametaka umakini katika utoaji wa tenda za ujenzi wa miradi mbalimbali ili kuepuka dosari.

Makonda ameyasema hayo leo, Jumamosi, Novemba 2, 2019, wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya kimkakati inayoendelea katika wilaya za Ilala na Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Makonda ametoa agizo kuwa Kampuni ya Nyanza inayosimamia mradi wa ujenzi wa Daraja la Mto Kivule isipewe tenda yoyote baada ya kukamilisha mradi huo, kutokana na kushindwa kukamilisha baadhi ya miradi ambayo wamewahi kupewa. Hata hivyo, Mkandarasi huyo tayari, ameanza ujenzi wa mradi huo baada ya kusikia RC Makonda anakwenda huko.


“Huyu mkandarasi huu uwe mradi wake wa mwisho katika Jiji la Dar es Salaam. Kama mnakumbuka hata Temeke aliwahi kufanya uzembe wa namna hii, vifaa hana vya kutosha kazi yenyewe haieleweki, tunataka Makandarasi wenye kasi kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesem Makonda.

Amesema baadhi ya Makandarasi wanapewa tenda na kuishia kulipa madeni yanayowakabili kutokana na fedha wanazoingiziwa kukatwa na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati.

“Mnapotoa hizi tenda mjiridhishe wengine ndio kama hawa ambao hadi leo kazi hazionekani,  pia msiwape kazi kwa rushwa mtashindwa kusimamia miradi hii muhimu kwa wananchi,” amesema Makonda



Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda, alitoa agizo la kuwekwa rumande kwa mkandarasi huyo kutokana na kusuasua kwa ujenzi huo.

Kwa upande mwingine, Mkandarasi anayejenga Machinjio ya Kisasa ya Vingunguti, Elisante Ulomi amesema, mradi wa machinjio ukikamilika utaongeza pato la Taifa kwa kuwa kila kitu kitakachoptoakana na zao la mifugo kitauzwa kwa mfano pembe, damu, ngozi, kwato na nyama ambapo Serikali itakusanya mapato na wananchi watafanya biashara kirahisi katika mazingira rafiki.

Katika hatua nyingine Makonda amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutokana na kasi ya utekelezaji wa mradi wa Machinjio ya kisasa katika eneo la Vingunguti jijini Dar es Salaam.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527