HUKUMU YA JAMAL MALINZI NA WENZAKE YAGONGA MWAMBA, HAKIMU KAHAMISHWA


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kusoma hukumu ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake watatu kwa sababu hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, Maila Kasonde amehamishwa kikazi.

Hukumu ya Malinzi na wenzake watatu ilitarajiwa kusomwa leo Novemba 7, 2019 na Hakimu Maira Kasonde.

Wakili wa Serikali wa TAKUKURU, Pendo Temu amemueleza Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kevin Mhina kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusomewa hukumu mbele ya Hakimu Kasonde lakini wamepata taarifa kuwa amehamishwa hivyo wanaomba muongozo.

Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mhina amedai kuwa ni kweli Hakimu Kasonde amepata uhamisho na taratibu za kumwezesha kuandika hukumu hiyo zimekamilika, hivyo anaahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21 mwaka huu 2019 ambapo hukumu inaweza kutolewa.

Awali kesi hiyo ilikuwa na mashtaka 30 lakini ilipofikia katika uamuzi wa kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama la walipunguziwa mashtaka 10 na kubakiwa na mashitaka 20.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ulikuwa na mashahidi 15 na vielelezo tisa.

Katika hatua hiyo mshtakiwa watano Miriam Zayumba aliachiwa huru kwa sababu kaonekana hana kesi ya kujibu kwa mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili.

Washtakiwa wengine waliobakia katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Katibu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 20 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527