CCM WAMPA ONYO BENARD MEMBE

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemuonya Benard Membe, kutokuwa juu ya katiba ya chama hicho.


Onyo hilo limetolewa leo  na Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM, wakati akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Konani kinachorushwa na Kituo cha ITV  kupitia mitandao yao ya kijamii.

Dk. Bashiru ameeleza kuwa, kama Membe ataendelea kutofuata utaratibu, uongozi wa chama hicho utamlazimisha kufuata utaratibu.


“Membe ni mwanachama mwenye haki ya kikatiba lakini ana wajibu. Kwa hiyo kama anataka kuwa mwanachama wa CCM kama walivyo wengine…  Asipofuata utaratibu, atalazimishwa kufuata utaratibu,” ameeleza Dk. Bashiru.

“Membe hayuko juu ya katiba, Mwalimu Nyerere aliasisi CCM na hakuwa juu ya katiba.  Membe akitaka kuwa mwanachama kama wengine wa CCM, afuate utaratibu, asipofuata mimi ndiye msimamizi wa utaratibu huo atalazimishwa kufuata utaratibu,” alisema.

Hata hivyo, amesema Membe hakuwahi kujadiliwa katika vikao vya chama, licha ya kwamba hakuitikia wito wake, alipomtaka kuonana naye akiwa mkoani Geita.

“Hatukuwahi kumjadili na kwenye vikao hakuwahi kufika. Kosa halifi kama jinai, kosa halifi unaweza ukadhani limekufa kumbe ni utaratibu wa wakati. Kupitia kwako, naomba kueleza wana CCM tuko makini kulinda utamaduni wa chama, na wanachama kutii viapo vyao,” amesema Dk. Bashiru.

“Nimekuja kuimarisha chama na hasa kufunga mitambo ya ushindi mwaka kesho, baada ya majaribio ya mitambo hiyo kufanya kazi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, natembea wilaya zote za Unguja na Pemba nikifunga mitambo,” amesema Bashiru.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post