KAMATI YA KITAIFA YA URATIBU NA UTHIBITI WA USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA YAZINDUA WIKI YA UHAMASISHAJI MATUMIZI SAHIHI YA ANTIBIOTIKI NCHINI

Na Andrew Chale
KAIMU Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliasi Kwesi amezindua rasmi  shughuli za kuhamasisha matumizi sahihi  ya dawa za Antibiotiki katika kuelekia wiki hiyo duniani itakayofanyika kuanzia Novemba 18-24, mwaka huu duniani kote.


Katika tukio hilo, Dkt. Kwesi  alimwakilisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu ambapo  alitaka jamii kuelewa athari na tatizo kubwa ambalo limekuwa likiongezeka duniani kote litokanalo na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

“Kuanzia tarehe 18-24 Novemba, mwaka huu, duniani kote tunaadhimisha  wiki ya kampeni ya dawa aina ya Antibiotiki (World Antibiotic Awareness Week).
Lengo ni kusisitiza na kuongeza uelewa juu ya matumizi sahihi ya dawa hizi ili kupunguza matumizi yasiyostahili na hatimaye kuzuia ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa hizi” alieleza Dkt. Kwesi.

Aidha,  alisema kuwa, Serikali imendaa mipango na miongozo mbalimbali ili kutekeleza kazi kwa usahihi ikiwemo mpango wa Taifa wa kupambana na usugu wa dawa dhidi ya vimelea mbalimbali Antimicrobial ( 2017-2022).

“Niwaagize  watoa dawa kote nchini kuandika  dawa kwa kufuata mwongozo  wa matibabu wa mwaka 2017 na kutumia majina halisi ya dawa (Generics). 

Pia naagiza vituo vyote vya huduma ya afya kutekeleza miongozo ya kukinga na kuzuia maambukizi  ambayo ni muhimu sana kwa kuzuia usugu katika sehemu zao  za kazi” alisema Dkt. Kwesi.

Aidha, akielezea ripoti ya  benki ya Dunia ya mwaka 2017 inabainisha kuwa zaidi ya watu 700,000 wanafariki kila mwaka kutokana na usugu  wa dawa.

“Hatua madhubuti zisipochukuliwa haraka zaidi  ya watu milioni 10 watafariki kila mwaka kutokana na usugu wa dawa ifikapo mwaka 2050.

Hali hii ya usugu wa vimelea inaweka mashaka makubwa ya kupoteza nguvu kazi ya Taifa hili kwa kusababisha vifo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyotibika kwa kutumia dawa zilizokuwa na uwezo wa kutibu, kuongezeka kwa umasikini  kutokana na kuugua muda mrefu na kutumia dawa ghari zaidi lakini pia  kuongezeka kwa vifo vya mifugo na udhalishaji hafifu wa chakula” alieleza Dkt. Kwesi.

Dkt. Kwesi alitoa wito kwa jamii kuzingatia matumizi sahihi  ya kuepukana hasa kwenye kinga ya maambukizi kwa njia ambazo zinaweza kufanywa mahali popote ikiwemo ngono salama, kuosha mikono na chanjo.

Hata hivyo Dkt. Kwesi alizitaka Wizara zingine wadau wakiwemo Mawaziri wa Mifugo na uvuvi,, Kilimo na Mazingira kwa pamoja kufanya kampeni zinazolenga kuongeza uelewa wa jamii juu ya matumizi sahihi na athari  zitokanazo na matumizi holela ya dawa kwa binadamu na mifugo.

Kwa upande wao wadau walioshiriki katika tukio hilo wakiwemo wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya (WHO), Shirika la Chakula (FAO) na Shirika la Wanyama (OIE) walieleza wanashirikiana kwa pamoja na Serikali ya Tanzania katika mapambano ya tatizo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post