KABATI AHOJI HALMASHAURI KUSHINDWA KUNUNUA MAFUTA MAALUM KWA WATU WENYE UALBINO

Na Halfani Akida - Dodoma

Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Iringa Mhe. Ritta Kabati  (CCM) amehoji uwepo wa baadhi ya halmashauri nchini kushindwa kununua mafuta maalumu ya watu wenye ualbino hali inayosababisha kuwa katika hatari ya kupata saratani hivyo kuitaka serikali kuchukua hatua kwa halmashauri hizo ili kuokoa maisha ya walemavu wa ngozi.


Kabati amehoji hayo Novemba 14,2019) katika mkutano wa kumi na saba wa vikao vya bunge vinavyoendelea jijini, Dodoma.

"Mahitaji makubwa maalum kwa walemavu wa ngozi ni mafuta maalumu ambayo yamekuwa yakiuzwa bei ghali sana, kwa kuwa serikali ilitoa agizo kwa halmashauri kununua mafuta hayo wakati zinapoagiza dawa, Je, nini kauli ya serikali kuhusu halmashauri zile zisizotimiza hitaji hili?",alihoji.


Mhe. Kabati alibainisha kuwa kundi la walemavu ni miongoni mwa makundi yenye uhitaji wa kupata huduma za afya bure, hivyo ameiomba serikali kulitambua kundi hilo muhimu katika jamii kwa kuwapatia vitambulisho vitakavyowawezesha kupata huduma za afya kama wazee.

Mhe. Kabati aliiomba serikali kuona haja ya kuwa na vitanda maalumu vya kujifungulia kwa walemavu katika hosptali za ngazi zote nchini ili kuepusha vifo vinavyojitokeza kutokana na ukosefu wa miundombinu sawia kwa watu wenye ulemavu.

"Vifo vingi vinatokea kutokana na ukosefu wa vitanda vya kujifungulia watu wenye ulemavu na miundombinu rafiki hospitalini, serikali inamkakati gani kuhakikisha tunazuia kutokea kwa vifo hivi, sambamba na kuboresha huduma za afya kwa watu wenye ulemavu nchini?",alisema.

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akijibu swali hilo alisema serikali inaboresha utaratibu wa msamaha wa matibabu kwa makundi yenye uhitaji wa msamaha kwa kuhakikisha wananchi wasio na uwezo tu wanapata msamaha.

"Wizara iliona ni vyema ikaboresha utaratibu kwa makundi yenye msamaha kwa kuhakikisha kuwa wananchi wasio na uwezo tu ndiyo wanapatiwa msamaha. Kwa sasa serikali inaendelea na maandalizi ya bima ya afya kwa wananchi wote, hivyo utaratibu utakapokamilika mswaada utawasilishwa bungeni",alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile alithibitisha uwepo wa hatari kwa walemavu wa ngozi kupata saratani ya ngozi kutokana na kukosa kinga madhubuti inayolinda ngozi zao.

 Hata hivyo, Mhe. Dkt. Ndugulile aliziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinabaini mahitaji ya walemavu wa ngozi na kununua mahitaji hayo.

"Ni kweli walemavu wa ngozi wapo katika hatari zaidi ya kupata saratani ya ngozi kutokana na kukosa kinga hii muhimu ya ngozi, Sisi kama serikali tuliwahi kutoa agizo kwa halmashauri zote nchini kununua mafuta hayo wakati wanapoagiza vifaa tiba, Hivyo, niendelee kuzikumbusha halmashauri kubaini mahitaji ya walemavu wa ngozi na kuhakikisha kwamba mafuta haya yanayowakinga walemavu wa ngozi yanakuwa ni sehemu ya viffa tiba vitakavyoagizwa",alisema.

Aidha, Dkt. Ndugulile alitoa maelekezo kwa bohari ya madawa kuhakikisha vitanda vinavyonunuliwa hospitalini viweze kuwa rafiki kwa makundi yote yaliyopo katika jamii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila kujali hali walizo nazo kimaumbile.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post