ALIYEKUWA RAIS WA KLABU YA SIMBA, EVANS AVEVA NA MAKAMU WAKE GODFREY NYANGE WAACHIWA KWA DHAMANA


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia kwa dhamana aliyekuwa Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange maarufu ‘Kaburu’.

Septemba mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa uamuzi wa kuwafutia mashtaka mawili ya utakatishaji wa fedha Aveva aliyekuwa rais wa simba na makamu wake Nyange, ambapo washtakiwa hao walitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh30 milioni kila mmoja, lakini upande wa Serikali ulikata rufaa kupinga dhamana hiyo.

Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba ameyatupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Serikali ya kupinga uamuzi huo.

Baada ya Hakimu Simba kutoa uamuzi huyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro alidai kuwa hawajaridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo, hivyo wanakwenda kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Uamuzi uliotolewa sijaridhika nayo, hivyo naenda leo hii kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania,” alidai Kimaro.

Baada ya Kimaro kueleza hayo Hakimu Simba alisema hata kama wanakata rufaa haitengui uamuzi wa mahakama hiyo na ndipo wakili huyo alipoieleza mahakama kuwa anajiondoa katika kesi hiyo, kisha Wakili Kimaro alinyanyuka na kutoka nje huku mahakama ikiwa inaendelea.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 12, 2019 itakapofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527