WIZARA YA KILIMO YAJA NA MKAKATI WA KUZALISHA MICHE MILIONI 20 YA KAHAWA

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kilimanjaro

Moja ya changamoto katika kuimarisha ubora wa Kahawa ni uzalishaji mdogo ya Miche ya Kahawa huku mahitaji yakiwa ni makubwa kwa wakulima.

Wizara ya Kilimo imekusudia kuzalisha mbegu mpya ambazo ni bora za kahawa kwa lengo kubwa la kubadilisha mikahawa ya zamani ipatayo milioni 240 kwa kutumia aina mpya za kahawa.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 21 Octoba 2019 wakati wa uzinduzi wa vitabu vya kanuni bora na mitaala ya ufundishaji katika zao la Kahawa katika Ofisi za Taasisi ya utafiti wa Kahawa TACRI Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa uzalishaji wa idadi ya miche milioni saba (7) kwa mwaka ni kidogo, ambapo itatuchukua takribani Miaka 35 kubadili aina hizi za zamani hivyo aliahidi kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa kilimo itahakikisha kunakuwa na mapinduzi ya Kilimo cha kahawa nchini.

Katika kuifikia dhamira ya kubadili mikahawa ya zamani serikali kupitia wizara ya kilimo imejipanga kuanza kuzalisha Miche milioni 20 ya kahawa mpya ili kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa.

Amesema kuwa sekta ndogo ya kahawa ina umuhimu mkubwa kwenye uchumi wa taifa na huchangia takribani asilimia 24 kwa mwaka ya mapato ya mauzo ya bidhaa za kilimo nje ya nchi, ambapo ni wastani wa asilimia 4 ya pato la taifa.

Hata hivyo, pamoja na mchango huo wa sekta ndogo ya kahawa uzalishaji bado ni mdogo sana, ambapo kwa mwaka wastani wa tani 50,000 huzalishwa.

Aliongeza kuwa hali hiyo inasababishwa na tija ndogo ambapo mpaka sasa mti mmoja wa kahawa unatoa gramu 250 ikilinganishwa na wastani wa gramu 1,000 inayotakiwa kuvunwa kwa mti.

Moja ya changamoto inayosababisha tija kuwa chini katika sekta ndogo ya kahawa ni ukosefu wa elimu ya kanuni bora ya kilimo cha kahawa kwa wakulima ambapo amewataka maafisa kilimo kote nchini kuanza kutoa elimu kwa wakulima juu ya umuhimu wa mikahawa mipya.

Alisema ili kuhakisha kuwa mkulima anapata tija kubwa na kuongeza kipato kutokana na kilimo cha kahawa, ni muhimu kupata elimu ya uzalishaji wa kahawa kwa kuzingatia matumizi sahihi ya kanuni bora za kilimo cha kahawa.

Waziri Hasunga ameipongeza TaCRI kwa kuandaa vitabu vilivyozinduliwa kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu kanuni bora za utunzaji wa kahawa aina ya Arabika na Robusta pamoja na mitaala ya mafunzo ambavyo vitatumika kwa Maafisa Ugani, Wakulima na Wananchi wote wenye nia ya kujifunza mbinu bora za kilimo cha kahawa chenye  tija.

Mhe Hasunga amesema kuwa Vitabu hivyo vyenye picha na maelezo ya kutosha vimelenga kuwapa wakulima wa kahawa utaalamu wa kukuza zao la kahawa katika lugha rahisi ambapo lengo la vitabu hivyo ni kuhakisha kuwa kaya za wakulima wa kahawa zipatazo 420,000 nchini; wanakuwa na rejea ya haraka na rahisi wakati wote wawapo shambani, mahali ambapo hawana wataalamu; na pale ambapo kutakuwa na mtaalamu vitakuwa vichocheo vya mazungumzo ili kuweza kujua zaidi au kupata ufafanuzi wa kitaalamu wa masuala ya kilimo cha kahawa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527