WANAFUNZI SHULE YA UGANGA WALIOKUMBWA NA MAPEPO WAMUUA MZEE WALIYEMTUHUMU KUWAROGA


Mzee Issa Pela enzi za uhai wake

Na Edwin Moshi - Njombe
Mzee Issa Pela anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (70-80) aliyekuwa miongoni mwa wanaotuhumiwa kwa ushirikina wa kuwaangusha wanafunzi wa shule ya msingi Uganga iliyopo kata ya Luwumbu wilayani Makete mkoani Njombe ameuawa kwa kupigwa wanafunzi wa shule hiyo.


Akizungumza na Malunde 1 blog Afisa mtendaji wa kijiji hicho Raphael Tweve amesema wanafunzi hao walianza kumkimbiza na kumpiga mzee huyo jana Oktoba 28, 2019, baada ya kuona hali hiyo aliwazuia lakini baadaye waliweza kumzunguka na kwenda kutekeleza kitendo hicho cha kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea umauti kwa mzee huyo.

“Mimi nikiwa ofisini nilisikia kelele nikatoka kwenda kuangalia kuna nini, kufika nawaona hao watoto akiwa na fimbo wanamtafuta mzee mwingine anayetuhumiwa kwa uchawi, na wakamweleza wameshampiga yule mzee waliyekatazwa wasimpige na alipokwenda eneo la tukio alimkuta mzee huyo amejeruhiwa kwa kipigo na baada ya muda mchache akafariki dunia” amesema Mtendaji huyo.

Amesema kwa sasa shughuli nyingi za maendeleo zimekwama kijijini hapo tangu Mei mwaka huu lilipoibuka suala la wanafunzi kudondoka ovyo shuleni hapo huku wakijaribu kutafuta muafaka bila mafanikio.

Kwa upande wa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo ambao majina yao tunayahifadhi wamesema kabla ya kutokea tukio hilo walimuona marehemu akionesha ishara za kishirikina kwenye nyumba za walimu shuleni hapo kwa kutumia kifimbo akiwa anachora ishara ya msalaba kwenye nyumba hizo huku akitoa maneno ya vitisho kuwa walimu hao watakufa.

Mmoja wa wanafunzi hao amesema kitendo hicho kiliwakasirisha na hata walipokuwa wakimuuliza alijibu kuwa hawamuwezi, huku wanafunzi wengine wakisema kuwa pia alichuma majani flani na akayaweka kwenye mfuko wa koti lake.

Wamesema walipoona hivyo ndipo walipolazimika kutafuta fimbo na kumfuata Mzee huyo kwa lengo la kumuadhibu ambapo alikiri kuhusika na vifo vya wananchi watatu kijijini hapo kwa njia za kishirikina.

“Sisi hatukuogopa kufa, kwani wamekufa wangapi, hata kama ni mchawi hatukuogopa kumpiga kwa kuogopa na sisi tungekufa”, amesema mwanafunzi mmoja.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Eliuda Msigwa amezungumzia namna mazingira yalivyokuwa kwa wanafunzi wake, pamoja na kushangazwa na uamuzi wa wanafunzi hao na kwamba baada ya kutokea tukio hilo la mauaji bado wanafunzi wakaendelea kuanguka shuleni hapo huku wakitaja kuwa wanafunzi hao wamehusika na mauaji hayo kwa taswira tu lakini sio uhalisia.

“Wapo wanafunzi wamedondoka leo na wakawa wanataja mambo ya ajabu, wanasema wamemchukua mwenzao (huyo marehemu) kwenda kumuhifadhi tu na wamemchukua kupitia wanafunzi hao, sasa hatufahamu ukweli ni upi kwani walikuwa wakizungumza hayo wanafunzi hao waliodondoka na mapepo”, amesema Mwalimu Mkuu huyo.

Mganga mfawidhi wa zahanati ya Uganga Frank Gavana amethibitisha kutokea kifo hicho baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu ambapo amesema majeraha ya sehemu za kichwa cha marehemu ni sababu kubwa iliyopelekea kifo chake.

Imeelezwa kuwa tangu mwezi wa tano mwaka huu kumekuwa na tabia ya kuanguka kwa wanafunzi katika shule ya msingi Uganga hali iliyopelekea watoto kushindwa kusoma kutokana na hali hiyo, pamoja na kuanguka watoto hao wamekuwa wakiwataja watu mbalimbali katika kijiji hicho kuwa ndiyo chanzo cha watoto kuanguka ambapo marehemu Mzee Issa Pila ni mmoja kati ya wanaotuhumiwa kufanya matukio hayo

Kwa upande wa serikali ya kijiji wakishirikiana na kata hiyo wameendesha vikao mbalimbali vya kutafutia ufumbuzi jambo hilo lakini hakuna mafanikio yoyote yaliyoweza kupatikana mpaka sasa.

Baadhi ya wanaotuhumiwa kutajwa na watoto hao pindi wanapodondoka wamekuwa wakiitwa kwenye vikao na kukiri kutafuta suluhu ya kumaliza tatizo hilo lakini hakuna mabadiliko mpaka sasa.

Jeshi la polisi wilaya ya Makete limefika eneo la tukio kwa hatua zaidi na kutoa elimu kwa wananchi hao na kuwataka kutochukua sheria mkononi huku pia wakiwaasa kuwa vitendo vya kishirikina kama hivyo vina madhara makubwa kwao kwa kuwa watumishi mbalimbali wanaopelekwa na serikali wataondoka kwa kuogopa ushirikina.

Juhudi za kumpata kamanda wa polisi Mkoa wa Njombe Hamisi Issa kuzungumzia tukio hilo zinaendelea baada ya Jana usiku kutafutwa bila mafanikio.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527