Serikali Kuwachukulia Hatua Kali Za Kinidhamu Watumishi Watakaobainika Kujihusisha Na Rushwa Ya Ngono | MALUNDE 1 BLOG

Tuesday, October 8, 2019

Serikali Kuwachukulia Hatua Kali Za Kinidhamu Watumishi Watakaobainika Kujihusisha Na Rushwa Ya Ngono

  Malunde       Tuesday, October 8, 2019
Na James K. Mwanamyoto, Tunduru
Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi wa umma watakaobainika kujihusisha na rushwa ya ngono katika maeneo yao ya kazi, kwani kitendo hicho kinadhalilisha na kushusha hadhi ya utumishi wa umma nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kilichofanyika wilayani humo jana kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Mhe. Mkuchika ametoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya Walimu wa shule za msingi wilayani Tunduru kushikiliwa na vyombo vya dola kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ya ngono jambo ambalo halileti taswira nzuri kwa umma, ikizingatiwa kuwa Walimu wana jukumu la kuwalea wanafunzi katika maadili mema.

“Inakuwaje Mwalimu unaepaswa kuwa mfano bora wa kuigwa kimaadili unataka rushwa ya ngono kwa mwanafunzi, kitendo hicho kinamuathiri mwanafunzi husika kitaaluma na kisaikolojia”, Mhe. Mkuchika amefafanua.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, hivi karibuni ofisi yake imesitisha ajira ya Mhadhiri mmoja wa chuo kikuu nchini, ambaye alituhumiwa na kubainika kuwaomba rushwa ya ngono wanafunzi wa kike ili waweze kufaulu mitihani yao kwa upendeleo.

“Wanafunzi wa kike wa chuo hicho waliandika barua ya malalamiko kwenye ofisi yangu na baada ya kuwahoji na kufanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vya dola ikabainika kuwa ni kweli hivyo akafukuzwa kazi,” Mhe. Mkuchika ameeleza.

Mhe. Mkuchika amewatahadharisha watumishi wa umma nchini kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iko kazini na ina utayari wa kumshughulikia mtumishi yeyote atakayetumia cheo chake vibaya ili kujinufaisha na rushwa ya ngono.

Aidha, Mhe. Mkuchika amesema nchi yetu imebahatika kuwa na viongozi wenye utashi wa kupambana na rushwa kuanzia Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere hadi Awamu hii ya Tano, inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amejipambanua kwa vitendo kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na Wahujumu Uchumi.


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post