MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WASHUKA HADI ASILIMIA 3.4

Na Mwandishi Wetu

Mfumuko wa Bei  wa Taifa kwa mwezi septemba, 2019 umepungua  hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.

Hayo yamesemwa na Kaimu mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja wakati akitangaza mfumuko wa bei jana Jijini Dodoma.

“Kushuka kwa mfumuko wa bei kunatokana na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwezi Septemba 2019 ikilinganishwa na bei za kipindi cha  Septemba,2018”. Alisisitiza Bi. Minja.

Akifafanua amesema kuwa baadhi ya bidhaa zilizopungua bei kwa mwezi Septemba ni mafuta ya taa asilimia 1.0, Petroli asilimia 3.3 ,majiko ya gesi asilimia 1.5, dawa za kuulia wadudu nyumbani asilimia 2.2 na mafuta ya nywele asilimia 1.3.

Aliongeza kuwa mfumuko wa Bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.

Akizungumzia nchi za Afrika Mashariki Bi. Minja amesema kuwa mfumuko wa Bei nchini Kenya  kwa mwezi Septemba umepungua hadi asilimia 3.83 kutoka 5.00 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.

Kwa upande wa nchi ya Uganda, mfumuko wa Bei kwa mwaka unaoishia mwezi Septemba 2019 umepungua hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka unaoishia mwezi Agosti, 2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527