MAHAKAMA KUTOA HUKUMU IJUMAA KESI YA ANAYEDAIWA KUMBAKA BINTI YAKE


Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepanga kutoa hukumu Ijumaa October 11,2019 dhidi ya Kigogo wa TPRI, Aresteric Silayo anayedaiwa kumbaka mwanae wa kike mwenye umri wa miaka 11.



Akizungumza mahakamani hapo juzi, Hakimu Mkazi Aziza Temu, aliyepewa mamlaka na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kusikiliza rufani ya kesi hiyo, alisema amesikiliza hoja za rufani hiyo za pande zote mbili.

"Baada ya kuwasikiliza upande wa utetezi na Jamuhuri, hukumu nitatoa Oktoba 11, mwaka huu," alisema.

Kabla ya hakimu Aziza kupanga tarehe hiyo, alimsikiliza Wakili wa Serikali, Azael Mwiteni, ambaye aliomba mahakama hiyo kutengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ya kumwachia huru mtuhumiwa huyo.

"Mheshimiwa naomba utengue uamuzi wa kumwachia huru mtuhumiwa huyu na kuzingatia ushahidi wa mtoto na mashahidi wote waliofika mahakamani hapa kutoa ushahidi unaofanana na usio na mashaka," aliiambia mahakama.

Alieleza ushahidi wa mtoto (jina tunalo) unaonyesha baba (mtuhumiwa) alimbaka mwanawe kwani mtoto aliweza kumweleza Mwalimu shuleni, mahakamani na pia cheti cha daktari aliyemchunguza amethibitisha mtoto huyo kubakwa.

"Kutokana na ushahidi uliotolewa Mheshimiwa utaona utakapopitia jalada hili kuwa mtoto ameeleza bila kubadili maneno, naomba mtie hatiani mshtakiwa na kumpa adhabu stahiki kulingana na kitendo alichokifanya kwa mwanawe.”

Naye Wakili wa Utetezi, John Materu, alidai hoja za Wakili wa Serikali hazina mashiko, kwani mahakama ilimwachia huru baada ya kuona ushahidi uliotolewa mahakamani ulikuwa wa shaka.

Alidai kesi hiyo ya kutengenezwa na ina sababu zake, hivyo hakuna ukweli wowote juu ya tukio hilo.
 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post