RAIS MAGUFULI AMPONGEZA MKUU WA MKOA WA MBEYA KWA KUWACHAPA VIBOKO WANAFUNZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa kuwarudisha nyumbani wanafunzi 392 wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya na kuwachapa viboko 14 wanaodaiwa kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo.

Jana Oktoba 3, 2019 Chalamila aliwachapa viboko wanafunzi hao kwa madai ya kuhusika kuchoma moto mabweni mawili ya shule yao, leo asubuhi Oktoba 4, 2019 akaagiza wanafunzi 392 kurudi nyumbani hadi Oktoba 28, 2019 wakiwa wamelipa Sh200,000 kila mmoja zitakazotumika kukarabati mabweni hayo. 

Wanafunzi 14 waliochapwa viboko wao wametakiwa kutoa Sh500,000 kila mmoja na kuripoti shuleni na wazazi wao huku wengine watano wakiendelea kushikiliwa na polisi kutokana na kutajwa kuhusika moja kwa moja na tukio hilo. Wanafunzi hao wanadaiwa kufanya kitendo hicho baada ya kukutwa na simu 29 kwenye mabweni. 

Akizungumza leo katika ziara yake mkoani Songwe, Rais Magufuli amesema viboko vinafundisha na kuwa ipo haja ya kufanyia marekebisho sheria inayozuia adhabu hiyo. 

“Leo nimeongea na Mkuu wa mkoa wa Mbeya na kumpongeza kwa kuwachapa wale wanafunzi viboko, yaani serikali inatoa fedha inajenga madarasa halafu hao wanafunzi wanayachoma, nimeagiza wale wanafunzi kidato cha tano na sita wote wafukuzwe na bodi ya shule ivunjwe”,amesema Rais Magufuli.

Amesema siku wanafunzi hao wakirejea shuleni lazima wazazi wao walipe fedha hizo kwa ajili ya kukarabati mabweni.

“Na wale wengine waliohusika kabisa peleka jela. Ndugu zangu nasema haya sio kwamba sina huruma nina upendo mkubwa na nimekuwa mwalimu nafahamu,” amesema Rais Magufuli.

“Nafikiri kama kuna mahali tulikosea ni ile sheria, inabidi ikafanyiwe marekebisho wawe wanatandikwa viboko.” 

“Eti mkuu wa mkoa anatandika viboko maana yake nini hata Ulaya wanatandika viboko,” amesema Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527