BAADA YA KUWACHARAZA VIBOKO WANAFUNZI...MKUU WA MKOA WA MBEYA AFUKUZA WANAFUNZI WOTE | MALUNDE 1 BLOG

Friday, October 4, 2019

BAADA YA KUWACHARAZA VIBOKO WANAFUNZI...MKUU WA MKOA WA MBEYA AFUKUZA WANAFUNZI WOTE

  Malunde       Friday, October 4, 2019
Na Esther Macha - Malunde1 blog Chunya
SIKU moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kuchapa viboko wanafunzi 14 wa shule ya sekondari Kiwanja wilayani Chunya kwa kosa la kumiliki simu za mkononi, Mkuu huyo wa mkoa amerejea tena shuleni hapo na kuwatimua wanafunzi wote 392 wa kidato cha tano na sita na kuwarejesha majumbani mwao.

Pamoja na adhabu hiyo, wanafunzi hao pia wanatakiwa kulipa shilingi 200,000 kila mmoja kwa wanafunzi 366 ambao hawakuhusishwa na tukio la uchomaji moto wa mabweni ya shule hiyo, huku wenzao 26 ambao ndio waliokamatwa na simu za mkononi wakitakiwa kulipa shilingi 500,000 kila mmoja, fedha ambazo zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili ya shule hiyo ambayo yalichomwa moto.

Akizungumza na wanafunzi hao jana, Chalamila alitoa muda wa saa nne kuanzia saa 1:00 hadi saa 4:00 asubuhi kwa wanafunzi hao kufungasha kila kilicho chao na kuondoka shuleni hapo.

Chalamila aliwataka kurejea Oktoba 18, mwaka huu wakiwa tayari wamelipa fedha hizo kupitia akaunti ya shule wakiwa pia na barua ya kukiri makosa yao na kuahidi kutorudia.

Alisema wanafunzi 26 ambao walikamatwa wakiwa na simu za mkononi, licha ya kulipa shilingi 500,000 kila mmoja siku ya kurejea shuleni wanatakiwa kufika na wazazi wao.

“Tumeamua kufunga kidato cha tano na Sita kwa sababu hakuna sehemu ya kulala, mabweni mliyokuwa mkilala ndiyo mmeyachoma moto,” alisema Chalamila.

Chalamila alisisitiza kuwa wanafunzi wote wanatakiwa kurejea shuleni Oktoba 18, mwaka huu akiwa amelipa kiasi hicho cha fedha huku akionya kuwa yeyote atakayekaidi Serikali itamfuata huko aliko na kumkamata.

Alisema hata kama mwanafunzi ambaye hatalipa fedha hizo akihamia shule za binafsi, atafuatwa huko na kuzuiwa kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha sita akiwa popote ndani ya mipaka ya Tanzania.

Alisema kuwa walimu waliokuwa wakifundisha kidato cha Sita pia wanapewa mapumziko kwa kipindi hicho ambacho wanafunzi watakuwa nyumbani.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi Maryprisca Mahundi aliwaasa wanafunzi hao kutekeleza maagizo yote waliyopewa ili waendelee kupata haki yao ya elimu.

Alisema kukaidi kutekeleza maagizo hayo kutasababisha wafukuzwe shule na kuzuiwa kufanya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mahali popote nchini.

“Maelekezo hayo hakikisheni mnayafanyia kazi kadri mnavyopewa, nje ya hapo mtajipotezea haki ya kusoma katika maisha yenu,” alisema Mahundi.

Baadhi ya wanafunzi walisema uamuzi huo unazidi kuwaongezea machungu kwa vile baadhi yao waliunguliwa na vitu vyao ndani ya mabweni na hawana namna ya kupata nauli za kurejea majumbani mwao.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post