HALOTEL TANZANIA YAONYWA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeitaka kampuni ya Simu ya Halotel nchini kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupeleka mawasiliano nje ya nchi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu na mwingiliano wa mawasiliano Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi ambapo alifika kwenye maunganisho ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo panatumika kupeleka mawasiliano kutoka nchini kwenda nchi jirani.

Akiwa kwenye maunganisho hayo, Nditiye alibaini kuwa kampuni ya simu ya Halotel imepeleka mawasiliano yake moja kwa moja kutoka nchini Tanzania kwenda nchi jirani ya Burundi kwa kuunganisha jozi za mawasiliano za kampuni hiyo kwenye Mfumo wa Mkongo wa Burundi (Burundi Backbone System) badala ya kufanya maunganisho hayo kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB)

“Nawaelekeza Halotel watumie Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupeleka mawasiliano nchi jirani ili kufuata utaratibu uliowekwa baina ya nchi moja na nyingine wa kuvusha mawasiliano yake kwenda nchi jirani kwa kutumia maunganisho ya Mkongo wa nchi moja kwenda maunganisho ya nchi nyingine badala ya kuunganisha mawasiliano kutoka kwa kampuni husika kwenda nchi nyingine moja kwa moja,” amesema Nditiye

Amefafanua kuwa Halotel hawaruhusiwi kufanya hivyo kwa kuwa wanakiuka utaratibu, wanaikosesha nchi mapato na inahatarisha usalama wa nchi kwa kuwa hakuna atakayeweza kufuatilia mawasiliano hayo upande wa pili kwenye nchi jirani

Naye Mhandisi wa Shirika la Mawasiliano (TTCL), Marwa Mwita amepokea maelekezo ya Nditiye na kukiri kuwa hakuna kampuni ya mawasiliano ya simu mkononi inayoruhusiwa kuvusha mawasiliano ya kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine bila kupitia Mkongo wa Taifa wa nchi husika kama vile Burundi, RBS; Rwanda, RDB na Tanzania, NICTBB.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Michael Mntenjele amemuarifu Nditiye kuwa wilaya hiyo na viunga vyake vinahitaji mawasiliano ya uhakika na yasiyokuwa na msongamano ili kufanikisha suala la ulinzi na usalama wa taifa letu kwa kuwa  wakazi waishio wilayani humo wako mpakani mwa Tanzania na nchi jirani za Burundi na Rwanda

Nditiye amemweleza Mntenjele kuwa Serikali imeielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia umoja wa kampuni za simu za Jumuiya ya Afrika (EACO) kudhibiti mwingiliano wa mawasiliano mpakani na kukubaliana kuwa hamna mtandao wa nchi moja kuingia kwenye nchi nyingine ili kila nchi ipate mawasiliano ya nchini kwake


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527