WANNE WATUPWA JELA MAISHA KWA KUKATA MKONO WA MTU MWENYE UALBINO KATAVI


Na Walter   Mguluchuma - Malunde 1 blog Katavi
  Watu wanne wakazi wa tarafa ya  Mamba Wilaya ya    Mlele  Mkoa wa  Katavi wamehukumiwa kwenda  jela  kifungo cha maisha baada ya  kupatikana na hatia  ya kutaka kumuua  mtu mwenye ualbino kwa kumkata mkono wake  na kisha kuondoka nao  kwa lengo la kwenda kuuza kwa mganga wa kienyeji.

 Waliohukumiwa  kifungo hicho cha  maisha kuanzia   jana   ni   Alex   Manyanza  Nogele  Maliganya , Galila  Nkuba (Malago) na   Shile  Dalushi wote wakazi wa  tarafa ya  Mamba  Wilaya ya   Mlele Mkoa wa  Katavi 

 Hukumu hiyo imetolewa  na  Jaji   Richard Wilbrod  Mashauri wa Mahakama kuu ya Kanda ya  Sumbawanga  katika  Mahakama ya  Hakimu  mkazi ya  Mkoa wa Katavi baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa  mahakamani  ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi kumi na mbili.

 Katika  kesi hiyo ilisikilizwa na   Mahakama kuu ya   Kanda ya  Sumbwanga upande wa mashitaka uliwakilishwa na wanasheria wa serikali wawili   Simon    Peres na  Dickson  Elias  Makoro na washitakiwa walitetewa na mawakili wawili  Elias Kifunda na  Patrick Mwakyusa.

  Awali katika kesi hiyo  waendesha  mashitaka wanasheria hao wa  serikali walidai kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja walidaiwa kutenda kosa hilo Mei  14 mwaka 2015 katika kijiji cha King'anda  tarafa ya Mamba majira ya saa sita usiku.

 Imelezwa kuwa siku ya tukio watuhumiwa hao  walikwenda nyumbani  kwao na  mtu  mwenye ualbino aitwaye  Lime   Luchoma  ambaye  alikuwa amelala  chumbani ndipo washitakiwa hao walipojaribu kumuua kwa kumkata  mkono wake wa kulia  na kisha kuondoka  na mkono huo kwa lengo la kwenda kuuza kwa mganga wa kienyeji kwa gharama ya shilingi milioni sita.

 Walidai kuwa baada ya kuwa wamechukua mkono wa  Lime Luchoma waliondoka nao na  kisha walikwenda kuubanika kwenye moto ili iwe   rahisi kwao kwa kuweza kuusafirisha na kwenda kuuza kwa mganga wa kienyeji aliyekuwa amewaagiza  wamtafutie.

 Katika  utetezi  wao  Mahakamani hapo washitakiwa hao waliiomba   Mahakama  iwaachie huru kwani  maelezo yao waliyoyatoa mbele ya  mlinzi wa  amani katika Mahakama ya  Mwanzo ya  Mpanda Mjini ambayo walikiri kufanya kitendo hicho  walidai walikubali kosa hilo kwa kuwa walikuwa wamepata mateso ya kupigwa na polisi.

Washtakiwa wote wanne wamepatika na hatia  ya kifungu  cha  sheria 211(a)  cha  sheria ya  adhabu  sura  namba 16   marekebisho ya mwaka 2002.

   Jaji  Mashauri alieleza kutokana na washitakiwa kupatikana na kosa hilo  Mahakama kuu    imewahukumu  washitakiwa hao wanne kutumikia jela kifungo cha maisha na kama hawajaridhika na hukumu hiyo wanayonafasi ya kukata rufaa.

  Katika kesi hiyo yenye washtakiwa sita,Mahakama  hiyo ilimwachia huru mshitakiwa wa sita  Masunga  Kashindye ambaye   baada ya kuachiwa alitimua mbio na kuelekea kusikojulikana ambapo mshitakiwa wa tano kwenye kesi hiyo   Maiko   Samweli  alifariki  dunia wakati akiwa mahabusu .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527