Full Time : YANGA 1-1 ZESCO UNITED, LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Yanga SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zesco United ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Matokeo yake yanamaanisha kwamba Yanga inatakiwa kwenda kufanya ilichokifanya kwenye Raundi ya kwanza kushinda ugenini baada ya sare kama hiyo nyumbani na Towsnhip Rollers ya Botswana mwezi uliopita. Yanga ilishinda 1-0 mjini Gaborone.
Katika mchezo wa leo, Yanga SC walitangulia kwa bao la mkwaju wa penalti la kiungo wake mshambuliaji, Patrick Sibomana dakika ya 24 akimchambua vizuri kipa wa kimataifa wa Zambia, Jacob Banda.

Refa Helder Martin Rodriguez aliyesaidiwa na washika vibendera Jeeson Emiliano dos Santos na Ivanildo Meirellesde O Sanche Lopes pamoja na Antonio Caluassi Dungula mezani alitoa penalti hiyo baada ya Marcel Kalonda kumchezea rafu Mnamibia wa Yanga, Sadney Urikhob.

Yanga walielekea kabisa kuondoka na ushindi katika mchezo wa leo kama makosa ya walinzi na kipa wao, Metacha Mnata kumruhusu kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Mzimbabwe Thabani Kamusoko kuisawazishai Zesco kwa shuti la mbali dakika ya 90 na ushei.

Ni bao ambalo liliwavunja nguvu Yanga na kujikuta wanacheza wakiomba mchezo umalizika kwa sare ya nyumbani. 

Yanga watajilaumu wenyewe kwa sare hiyo, kwani walitengeneza nafasi nzuri za kufunga, lakini wakashindwa kuzitumia.

Timu hizo zitarudiana Septemba 27, mwaka huu mjini Ndola na mshindi wa jumla ataingia hatua ya makundi, wakati atakayefungwa ataangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. 

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Mapinduzi Balama/Ali Ali dk74, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Mohammed Issa ‘Banka’/Mrisho Ngassa dk58, Abdulaziz Makame, Papy Kabamba Tshishimbi, Sadney Urikhob/Maybin Kalengo dk58 na Patrick Sibomana.
 
Zesco United; Jacob Banda, Marcel Kalonda, Simon Silwimba, Anthony Akumu, John Ching'andu/Kondwani Mtonga dk64, Kasumba Umaru/ Quadri alaedekoun dk73, Thabani Kamusoko, Enock Subumukama/Winston Kalengo dk37, Jesse Were, Mwila Phiri na Clement Mulashi.

Via>> Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527