WADAU WA ELIMU WAKUTANA KUFANYA TATHMINI YA UTEKELEZAJI MALENGO YA MWAKA


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknologia, Dkt Leonard Akwilapo, amesema serikali imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha inaboresha hali ya Elimu hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha miondombinu na kupitia mitaala kama inatija kwa wakati wa Sasa.

Dkt Akwilapo ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathmini uliowakutanisha wizara ya Elimu na wadau wengine wa elimu pamoja na asasi za kiraia ambazo ni wadau wa elimu, na wafadhili wanaokutana kwa siku tatu kutoa taarifa na kutathmini malengo waliojiwekea katika kuboresha elimu.

Amesema Wizara imekuwa ikifanya jitihada za maksudi kuhakikisha kiwango cha elimu kinakuwa na kutoa elimu yenye ubora, na wameanza kuboresha miondombinu ya vyuo ya Elimu ya juu, Kati na shule zote msingi na sekondari ili maboresho hayo yaendane na miondombinu ili kufanikisha adhima hiyo.

"Serikali tumekuwa tukijitahidi kuboresha hali ya Elimu yetu, utaona kwa Sasa tumeanza kuboresha miondombinu ili tunapotaka elimu iwe bora na miondombinu iwe bora kwa wanafunzi wetu, utaona tumeboresha vyuo vya Mzumbe, UDSM, sambamba na uboreshaji Madarasa kwa vyuo vya Kati na shule zetu zote" amesema Dkt Akwilapo.

Pia amebainisha maboresho hayo yanaenda sambamba na mitaala katika shule zetu na vyuo tunataka iendane na matakwa ya wakati wa sasa ili mwanafunzi anapotoka aweze kujitegemea tofauti na sasa wanategemea kuajiriwa.

Amesema kupitia mkutano huo kwa kushirikisha na wadau hao watajadili na kutoa taarifa ya utekelezaji wa malengo waliojiwekea katika mkutano uliopita, kwa kuangalia mafanikio na  changamoto katika kutekeleza malengo hayo.

Kuhusu kiwango cha elimu hapa nchini amesema imeimalika tofauti na mawazo ya watu wanaofikilia kuwa ipo chini, amesema kwa wanafunzi wanaomaliza sekondari hapa nchini akienda nje kwa elimu ya juu wanafanya vizuri,hata katika mashindano mbalimbali ya nje ya nchi wanafunzi wa Tanzania wamekuwa wakifanya vizuri.

Aidha ametumia mda huo kuwapongeza wanafunzi wa wawili wa chuo cha DIT, waliofanya vizuri na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Africa Techoology Challenges, ambapo Kama nchi tulishika nafasi ya pili kati ya nchi  za Afrika, na kwa mtu mmojammoja, Christopher Mbembela, alishika nafasi ya pili, na Apollo Maturo kushika nafasi ya tatu kati ya wanafunzi wa nchi zilizoshiriki mashindano hayo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtandao wa Asasi za kiraia ambao ni wadau wa elimu, TENMET, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hakielimu, John Kalaghe, amesema wao kama wadau wa elimu wanaridhishwa na hali ya Elimu hapa nchini hasa katika udahili kwa wanafunzi msingi umeongezeka, hata wale wa msingi kwenda sekondari.

" Sisi Kama wadau wa elimu tunaipongeza Sana serikali kwa kuamua kutoa elimu bite hii imeongeza sana kuongeza hamasa kwa watoto kusoma, hata ukiangalia usawa wa kijinsia katika udahili sasa unaridhisha Sana kwa sasa" amesema Kalaghe.

Amesema wao kama wadau kupitia mkutano huo wataangalia na kushirikishana changamoto zilizopo katika elimu hasa kuangalia kuongezeka kwa udahili katika shule kusiathiri kutolewa kwa elimu iliyobora kwa watoto wetu. 



 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527