DC NDAGALA AWATAKA WANANCHI KUSITISHA SHUGHULI ZA KILIMO WAKAPIGE KURA


Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala

Na Rhoda Ezekiel - Malunde 1 blog 
Wananchi wilayani Kakonko Mkoani Kigoma wametakiwa  kuacha tabia ya kwenda kwenye shughuli za kilimo wakati wa uchaguzi ili kufika katika vituo kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo na kuepuka kuchaguliwa viongozi wanaotafuta uongozi kwa matakwa yao binafsi.

Wito huo umetolewa  jana na Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala, wakati akiwahamashisha wananchi hao kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika wa  serikali za mitaa utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi hao pia kuhakikisha kuwa wanachagua viongozi waadilifu, wasiopenda rushwa bali wapenda maendeleo na kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo analoliongoza.

"Kumekuwepo tabia ya wananchi wengi vijijini kutoshiriki katika chaguzi mbalimbali hususani wakati huu msimu wa kilimo ambapo wananchi wengi wanahamia mashambani. Ni vyema wananchi kutenga muda wa kushiriki katika kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao",alisema.

Aidha aliwaonya baadhi ya viongozi wa vijiji vilivyoko mpakani wanaojihusisha na vitendo rushwa kwa kugawa ardhi kwa wananchi ambao inasadikiwa siyo raia wa Tanzani na kushiriki kuhifadhi mifugo yao na pia kuwanyanyasa wananchi. 

"Nitoe wito kwenu wananchi ni haki ya kila raia kushiriki katika uchaguzi iwe kuchaguliwa au kuchagua. Tukijitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi itatusaidia kupata viongozi watakao tuongoza katika misingi ya uadilifu na uwajibikaji, ni jukumu letu kuhakikisha uchaguzi huu tunatenda haki, tuhudhurie mikutano ya wagombea na tusikilize sera zao ili kujua ni kiongozi gani anatufaa',aliongeza Kanali Ndagala.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kakonko Masumbuko Magang'hila aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kuweza kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi.

Alisema zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura litahusisha wale ambao hawakujiandikisha katika daftari la awali la kupigia kura, waliofikia umri wa kupiga kura, waliopotelewa vitambulisho vyao na waliohama makazi yao ya mwanzo na kuhamia sehemu ambayo hawakujiandikishia.

Alieleza kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu na watakaoshiriki ni wale waliojiandikisha, na wale ambao wanasifa za kugombea na kuwataka wananchi wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali na wasiogope.

Naye Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Kakonko, Ladisraus Ibrahim Msaki aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa yeyote atakaye kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa kwa ajili ya kupata uongozi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na kuepuka kupata viongozi wasiofaa watakaokuwa wapenda rushwa na wasiopenda maendeleo.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Joackim Antony ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kabingo alisema wanatambua ni haki ya kila mwananchi kushiriki katika uchaguzi na wao kama vijana watahakikisha wanashiriki kikamilifu kuhakikisha wanapata viongozi walio bora.

Alisema changamoto inayowakatisha tamaa ni pale wanapochagua viongozi halafu wanajitokeza baadhi wanawapitisha wagombea wanaowataka wao bila kushinda hivyo kuiomba serikali kuwa makini katika uchaguzi huu ili kuweza kuondokana na changamoto hizo.

Nezia Kasiano ni Mwananchi Katika Kijiji cha Kabingo alisema watahakikisha wanashiriki katika uchaguzi huo na kwamba hakuna jambo litakalowazuia kushiriki, endapo watapata viongozi wazuri itawasaidia hata kupanga mipango ya maendeleo katika vijiji vyao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post