TOZO YA MAITI HOSPITALINI YAZUA GUMZO BUNGENI

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Suala la utozaji gharama miili ya Marehemu kwenye chumba cha kuhifadhia Maiti hospitalini [Mortuary] imeonesha bado ni changamoto kubwa kwa jamii masikini ambapo Bunge limeiomba serikali kuangalia upya Sera hiyo.


Akihoji suala hilo ,Mbunge wa Viti Maalum Suzan Lyimo amehoji ni lini Serikali itaacha kutoza gharama za Marehemu wanaofia hospitalini na kuhifadhiwa katika vyumba vya maiti[Mortuary] ili kupunguza simanzi kwa wafiwa.

Mhe.Lyimo amesema watu wengi ni Masikini Wanawezaje kulipia gharama kubwa na imekuwa changamoto kwao pindi miili ya ndugu zao inapozuiliwa kwa kukosa gharama ya kulipia gharama ya chumba cha kuhifadhia Maiti.

Katika Majibu yake Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Dokta Faustine Ndugulile amesema ili miili ya Marehemu wanaofia hospitalini au nje ya hospitali iweze kuhifadhiwa na kusitiriwa kwa heshima ,inahitaji kutunzwa kwenye majokofu yenye ubaridi mkali  na wakati mwingine kuwekewa dawa ili isiharibike.

Hivyo,Dokta Ndugulile amefafanua kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Mwaka 2017 ,wananchi wanapaswa kuchangia gharama za afya ikiwa ni pamoja na matibabu na hata huduma za uhifadhi wa maiti.

Dokta Ndugulile ameendelea kufafanua kuwa panapotokea changamoto ya mwananchi kushindwa kumudu gharama anapaswa kutoa taarifa kwenye uongozi wa hospitali husika au ofisi za ustawi wa jamii  ili kupata maelekezo ya namna ya kutatua changamoto hiyo huku pia akisisitiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya.

Kwa upande mbunge wa Viti Maalum  Mhe.Faida Bakari katika swali lake la nyongeza amehoji kama serikali inazuia Maiti  hospitalini kisa kushindwa kulipia gharama za Chumba cha kuhifadhia Maiti je inawapeleka wapi.

Akijibu swali hilo,Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amesema kikubwa ambacho serikali hudai ni gharama za mgonjwa alizolazwa hospitalini  hadi anapopona au kufariki .

Mwenyekiti wa Bunge Mhe.Nagma Giga ameitaka serikali kuangalia upya sera ya utozaji maiti hospitalini hususan suala la kupandisha bili pindi mtu anapochelewa kuchukua mwili wa Marehemu Mortuary hali hiyo itaweza kuondoa ukakasi ,Majonzi na Sintofahamu kwa wananchi.

Ikumbukwe kuwa gharama za kumlaza Mgonjwa kwenye chumba cha wagonjwa Mahututi [Intesive Care Unit]ICU]ni Tsh.laki tano[500,000] kwa hospitali za serikali na  Tsh.Milioni mbili na nusu[2,500,000] kwa hospitali za Watu Binafsi


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post