TAARIFA KWA UMMA JUU YA KUTOKEA KWA TETEMEKO LA ARDHI KATIKA MKOA KATAVI


Mnamo tarehe 9/09/2019 majira ya saa 9:38 usiku kumetokea tetemeko la ardhi katika kijiji cha Sibwesa Kata ya Sibwesa karibu na ziwa Tanganyika katika mkoa wa Katavi Wilayani Mpanda DC (Wilaya ya Tanganyika). 

Taarifa zilizokusanywa na kuchakatwa kutoka kwenye kituo cha kuratibu matetemeko ya ardhi kilichopo Dodoma katika ofisi za Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), zinaonesha kuwa tetemeko hilo lina ukubwa wa 5.5 katika kipimo cha Ritcher. 

Kitovu cha tetemeko hilo  kipo umbali wa kilometa 35.5 Kusini– Magharibi ya mji wa Mpanda kwenye latitude 6.47°S na longitude 30.77°E.  Eneo hili lipo katika ukanda wa bonde la ufa la Afrika Mashariki, mkondo wa Magharibi ambao ni njia kubwa ya matetemeko ya ardhi. 

Kwa taarifa tulizozipata kutoka kwa mashuhuda mbalimbali, tetemeko hili limesikika katika maeneo ya miji ya Mpanda, Mpanda DC na Sumbawanga.

Ukubwa wa tetemeko hili la ardhi kitaalamu ni tetemeko linaloweza kuwafanya watu waliolisikia kukimbia kwa hofu toka nje ya majengo, kusababisha uharibifu wa majengo kutegemeana na ubora wa majengo hayo.

Hadi sasa, GST imepokea taarifa ya baadhi ya nyumba kuwa na nyufa katika Kata ya Sibwesa na nyumba mmoja katika Kata ya Mishamo kijiji cha Isenga  imebomoka na kujeruhi mtoto. 

GST inaendelea kuwatahadharisha wananchi juu ya kuzingatia ujenzi wa nyumba imara zinazoweza kukabiliana na athari za matetemeko ya ardhi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza. Pia wananchi wanaombwa kuacha kutaharuki wakati wa tetemeko kwa kukimbia kwani inaweza kusababisha madhara mengine ya kuumizana na kupata mshtuko.

Imetolewa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
9/09/2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527