Na Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Jumla ya madaktari bingwa 365 wanatarajia kuhitimu mafunzo kuanzia mwaka wa wasomo 2019/2020, 2020/2021 na 2021/2022 ambao watasambazwa kwenye hospitali mbalimbali nchini kulingana na uwiano wa wataalamu waliopo pamoja na kuzingatia maeneo yenye uhaba mkubwa.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile amesema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Sonia Jumaa Magogo juu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza Madaktari Bingwa nchini.
“Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa katika ngazi mbalimbali za huduma nchini ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” amesema Dkt. Ndugulile.
Ameendelea kusema kuwa katika mwaka 2017/2018, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 2 zilizotumika kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa 125 wa fani za kipaumbele katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ambao wanatarajia kumaliza 2020/2021.
Aidha, katika mwaka 2018/2019, Serikali ilitenga kiasi cha Shilingi bilioni 1.8 ili kuendelea kugharamia mafunzo ngazi ya kibingwa katika kada mbalimbali za afya 127 katika Chuo cha MUHAS.
Dkt. Faustine amesema, katika mwaka 2019/2020, Wizara imetenga jumla ya shilingi 1,844,617,090 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya wataalamu bingwa katika fani za vipaumbele.
“Kutokana na uhaba uliopo kwenye hospitali za Rufaa za Mikoa, Wizara itahakikisha fedha hii inatumika vyema katika kusomesha wataalamu wanaotoka kwenye maeneo yenye uhaba mkubwa,” amesema Dkt. Ndugulile.
Aidha, wizara kupitia hospitali za rufaa ngazi ya Taifa na Taasisi za nje zitaendelea kuendesha kambi za udaktari bingwa hapa nchini, kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa na kujenga uwezo wa wataalamu.