OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAADHIMISHA SIKU YA TABAKA LA OZONI DUNIANI


Utafiti wa kisayansi katika tabaka la ozoni katika karne ya ishirini ulithibitisha kumong’onyoka kwa  tabaka hilo kutokana na kulundikana angani kwa kemikali aina ya chloroflourocarbons (CFCs), halons, methyl choroform, methyl bromide, carbon tertrachoridena nyinginezo. 


Hayo yalisemwa na Mkuu wa Chuo cha VETA– Chang’ombe Bi Vaileth Mfumbwa wakati wa warsha ya mafunzo kwa Mafundi mchundo wanaoshughulikia majokofu na viyoyozi  ikiwa ni maadhimisho ya siku ya tabaka la ozoni Duniani  iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, iliyofanyika katika Chuo cha VETA-Chang’ombe jijini Dar Es Salaam.

Aliongeza kuwa Kemikali hizi hutumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, ushafishaji chuma, utengenezaji wa magodoro, madawa na manukato ya kupulizia, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku na mashamba ya maua na ufukizaji wa mazao katika maghala kabla ya kusafirishwa nje ya nchi. Matumizi ya kemikali hizi yapo kwa wingi katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea, kama Tanzania.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bi Kemilembe Mutasa  alisema kuwa , Kitaifa maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yanafanyika jijini Dar es Salaam ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wakufunzi wa Chuo cha Ufundi Dar es salaam wamepanga kutoa mafunzo kwa vitendo kwa mafundi mchundo wanaohudumia majokofu na viyoyozi kuhusu njia bora za kuhudumia vifaa hivyo; kutoa elimu jinsi ya kutumia vitambuzi vya gesi; na kubadilisha tekinolojia zinazotumia kemikali haribifu kwa tabaka la Ozoni kwa kemikali mbadala. 

“Katika maadhimisho haya, tunakumbushwa kuwa katika Mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Monteral uliofanyika nchini Rwanda mwaka 2016, nchi wanachama zilikubaliana kupunguza uzalishaji na utumiaji wa  kemikali jamii ya Hydrofluorocarbons (HFCs) ambazo pia hujulikana kama R-143a kwa jina la biashara  na kukubaliana kuzuia ongezeko la joto la dunia kwa nyuzi joto 0.5 (0.5 degrees Celsius)” alisema Bi. Mutasa 

Warsha hiyo ya mafunzo ya siku moja imekua chachu kwa Mafundi Mchundo wanaoshughulikia majokofu na viyoyozi kwa kufundishwa njia mbalimbali za kiutaalamu za kutumia wanapokua katika shughuli zao za kila siku.  Mafunzo hayo yalitolewa na Wakufunzi wa Chuo cha Ufundi-VETA Chang’ombe jijini Dar Es Salaam.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527