KIJANA AMUUA KWA KUMPIGA RISASI BABA YAKE AKIDHANI NI NGURUWE


Polisi nchini Italia wamefungulia mashtaka ya kuua bila kukusudia bwana mmoja ambaye alimpiga risasi mpaka kufa baba yake wakiwa mawindoni.

Wawili hao, walikuwa katika mawindo ya kitoweo aina ya ngiri (nguruwe pole) mkasa huo ulipotokea jana Jumapili.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, baba na mwana walikuwa katikati ya kichaka karibu na mji wa Postiglione katika jimbo la kusini la Salerno.

Mtoto huyo, mwenye miaka 34, alifyatua risasi alipoona kivuli kisha majani kutikisika ghafla, akidhani ni ngiri. Kumbe alikuwa baba mtu, na risasi ilimpata chini ya tumbo.

Kijana huyo alipiga mayowe haraka baada ya kugundua kilichotokea huku akijaribu kumpatia msaada mzazi wake.

Hata hivyo, madaktari walishindwa kuokoa maisha ya bwana Martino Gaudioso aliyekuwa na miaka 55.

Wawili hao walikuwa wakiwinda kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ambalo ni marufuku kufanya shughuli za uwindaji.

Wanaharakati wa haki za wanyama wanaeleza kuwa matukio ya uwindaji haramu nchini Italia yamefikia kiwango kibaya.

"Ni dharura kubwa ya kitaifa," mwanaharakati kinara Michela Vittoria Bambira amesema.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Sergio Costa, waziri wa mazingira wa Italia alipiga marufuku ya kitaifa ya mawindo ya siku ya Jumapili baada ya kijana wa miaka 18 kupigwa risasi na kuuawa katika mpaka na Ufaransa.

Mpaka kufikia mwish0 wa mwezi huo, watu wawili zaidi (mmoja mika 26 mwengine 56), waliuawa katika mazingira ya namna hiyo.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527