NAIBU WAZIRI WA FEDHA: SIJARIDHISHWA NA UTENDAJI WA OFISI YA MKURUGENZI KONDOA


Na Josephine Majura, Kondoa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa muda wa siku 37 kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha kuwa ujenzi wa vituo vitatu vya afya vya Bereko, Thawi na Kalamba vinakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Dkt. Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, ametoa maagizo hayo alipofanya ziara ya kutembelea mradi ya ujenzi wa vituo vya afya vinavyojengwa kwa fedha za Serikali katika vijiji mbalimbali Wilayani Kondoa, mkoani Dodoma, ambapo alibaini kuna uzembe katika umaliziaji wa ujenzi wa baadhi ya vituo hivyo  kikiwemo Kituo cha Afya Kalamba.

Alielezea kutoridhika na utendajikazi wa  uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo katika usimamizi wa miradi hiyo muhimu kwa wananchi wakati Serikali ilikwishatoa fedha zote za kukamilisha miradi hiyo na kuagiza hadi Oktoba 30 mwaka huu miradi hiyo iwe imekamilika.

 “Dhamira njema ya Serikali  ya Awamu ya Tano ya Rais  Mhe. Dkt. John Joseph Pombe  Magufuli yakuleta milioni 400 kwenye kituo hichi cha Afya ni kupata huduma lakini hatujaanza kutoa huduma hiyo  kwa zaidi ya mwaka sasa”, alisema Dkt. Kijaji.

Aliiagiza Ofisi ya Mkoa na Wilaya hukakikisha wanafuatilia vizuri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi inayofadhiliwa na Serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwa sababu Serikali haianzishi mradi mpya bila kutoa fedha zote za miradi husika.

Serikali ilitoa fedha kwa nyakati tofauti kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa vituo vya afya vitano wilayani Kondoa kati ya vituo hivyo, vituo viwili vya Mauno na Busi vimekamilika, huku vituo vitatu vya afya vya Bereko, Thawi na Kalamba havijakamilika.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kondoa Bw. Mashauri Vicent alimuahidi Dkt. Kijaji kutekeleza magizo yote aliyoyatoa hasa ya kulipwa kwa watumishi waliofanya kazi mbalimbali kwenye vituo hivyo vya afya ndani ya siku 14.

Naye Mwanakijiji wa Mauno Bw. Haji Selemani, ameishukuru Serikali kwa juhudi mbalimbali inayofanya katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa huduma za jamii na kusifia huduma inayotolewa na Watumishi wa Kituo cha Afya Busi.

Kwa upande wake Mwanakijiji cha Bereko Bw. Juma Saidi amempongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi kubwa anayoifanya jimboni huko na kumuombea afya njema ili awe na nguvu yakufanya kazi na zaidi.

Dkt. Ashatu Kijaji alikuwa kwenye ziara ya siku mbili wilayani Kondoa, mkoani Dodoma ambapo ametembelea mradi wa Ujenzi wa vituo  vitano vya  afya  wilayani huyo ambavyo vinajengwa kwa fedha za Serikali na kuahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Wakazi wa Wilaya ya Kondoa.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527