Breaking : ROBERT MUGABE AFARIKI DUNIA


Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe (95) amefariki dunia.

Mugabe alikuwa nchini Singapore akipokea matibabu kwa muda mrefu.

Ameiongoza Zimbabwe kutoka 1980 mpaka 2017, alipong'olewa madarakani na makamo wake kwa msaada wa jeshi.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa tayari amethibitisha kupitia mtandao wa twitter juu ya taarifa za kifo hicho.
"Kamarada Mugabe alikuwa ni mwanga wa mapinduzi, mwana umajui wa Afrika ambaye aliyatoa maisha yake katika ukombozi na kuwawezesha watu wake. Mchango wake kwa taifa letu na bara (la Afrika) hautasahaulika..." ameandika Mnangagwa.

Mugabe alizaliwa Februari 21, 1924 kwenye koloni la Rhodesia.

Alitupwa jela kwa miaka 10 bila ya kufunguliwa mashtaka kwa kuukosoa uongozi wa Rhodesia mwaka 1964.

Mwaka 1973, yungali gerezani alichaguliwa kuwa raisi wa chama cha Zimbabwe African Union (Zanu), ambacho alikuwa ni mwanachama mwanzilishi.

Baada ya kuachiwa kutoka gerezani, alikimbilia Msumbiji na kuongoza mapambano ya kijeshi ya kudai uhuru.

Licha ya kuwa mpiganaji wa vita vya kushtukiza, alisifika kwa kuwa mzuri kwenye majadiliano.

Mwaka 1980 akafanikiwa kuingia madarakani baada ya uchaguzi uliomaliza utawala wa walowezi wachache wa kizungu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527