MGEJA AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KUMSAMEHE NAPENape Nnauye na Khamis Mgeja (kulia)

Na Raymond Mihayo - Kahama
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa uamuzi wake wa utu wa kumsamehe aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ambaye hivi sasa ni mbunge wa jimbo la Mtama,Nape Nnauye.

Mgeja  ametoa pongezi hizo leo Jumatano Septemba 11,2019 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akiwa shambani kwake akiandaa Mashamba kwa ajili ya msimu huu wa Kilimo katika kijiji  cha Nyanhembe kata ya Kilago Wilayani Kahama.

Alisema  kitendo kilichofanywa na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Dkt. John Magufuli cha kuwasamehe waliomkosea na waliotangulia hivi karibuni kuomba radhi wakiwemo January Makamba na William Ngeleja na hata wengine ambao wamekuwa wakiomba kimya kimya na kwa maandishi ni jambo bora na heshima kwa kila kiongozi na wasio viongozi kuiga mfano huo wa utu na ubinadamu

Mgeja pia alimpongeza Mbunge huyo wa Mtama Nape Nauye kwa kujitathimini na kuona mapungufu yake na matendo yaliyoondoa heshima na utu mbele ya kiongozi wa nchi na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa.

Alisema kitendo alichokifanya Nape cha kukaa chini na kujitathimini na hatimaye kuchukua hatua ya kwenda Ikulu kumuomba radhi Rais Dkt. John Magufuli ni cha ujasiri na unyenyekevu wa mtu mwenye utu.

Mgeja alisema amefurahishwa na kitendo hicho na kwamba ana imani Watanzania wengi wamefurahishwa na kitendo cha Nape kugundua mapungufu na makosa yake mbele ya kiongozi wa Nchi na Mwenyekiti wa CCM Taifa.

"Nampongeza Rais Magufuli kwa kuendelea siku zote kutufundisha na kutupa somo na kutuonyesha njia Watanzania kwa mambo mengi ya msingi ambayo kwa kiongozi yeyote anapaswa kuwa nayo na kuyaishi na kutolea mfano uadilifu, uwazi, ukweli na hili kubwa sasa la KichaMungu na kujenga utamaduni wa kusamehe ambalo linatija na afya katika maisha ya kila binadamu hapa duniani",alisema Mgeja.

Hata hivyo Mgeja alisema  suala la kusamehe limehimizwa hata katika vitabu vyote vitakatifu vya Dini na Mwenyezi Mungu jambo kama hilo linamfurahisha sana na lina baraka kubwa ndani yake.
:
"Katika Dunia hii, Maisha tunayoishi hakuna mwanadamu asiyekuwa na makosa ndiyo maana watu tunaenda Misikitini na Makanisani, na ni muhimu binadamu kugundua makosa yake ili upate nafasi ya kutubu na kujirekebisha ili upate kusamehewa na Mwenyezi Mungu',aliongeza.

Alitoa wito kwa baadhi ya viongozi wengine na hasa wanasiasa wajenge utamaduni wa kusamehe kwani wengi wao sio wawazi na wakweli huwa wamejaza vinyongo na chuki kwenye vifua vyao na kuchekeana kinafiki tu na jambo la kusamehe ni gumu sana kwao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post