MBOWE NA WENZAKE 8 WASHINDWA KUJITETEA MAHAKAMANI.....KESI YAPIGWA KALENDA


Viongozi 9 wa CHADEMA, akiwemo Mwenyekiti  wake Freeman Mbowe wameshindwa kuanza kujitetea katika kesi ya uchochezi inayowakabili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sababu mawakili wanaowatetea wanasimamia kesi Mahakama Kuu ya Tanzania.

 

Leo viongozi hao 9 walitarajia kuanza kujitetea baada ya Mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu kutokana na ushahidi wa mashahidi 8 uliofungwa na Upande wa Mashitaka.

Wakili Gaston Garubindi amedai hayo leo Jumanne Septemba 17, 2019  akieleza kuwa maelekezo aliyopewa na wakili Peter Kibatala anaomba shauri hilo liahirishwe.

"Wakili Profesa Safari (Abdallah) yuko Mahakama Kuu Shinyanga mbele ya Jaji Mkeha na Kibatala yuko Mahakama Kuu mbele ya Jaji Tiganga baada  ya kupata wito wa dharura jana kutakiwa afike mahakamani hapo leo,” amedai wakili Garubindi.

Wakili Garubindi amedai wakili mwingine katika kesi hiyo, Hekima Mwasipu yuko Mahakama Kuu Tanga kwenye kesi ya madai namba 7/2019 mbele ya Jaji Mruma.

Sababu nyingine iliyoelezwa na wakili Garubindi ni mshtakiwa wa pili, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji  Peter Msigwa na mshtakiwa wa nane, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche wamefiwa na ndugu zao hivyo wanafanya taratibu za kwenda kwenye mazishi.

Wakili mkuu wa Serikali, Faraji Nchimbi alipinga sababu hizo kutokana na kutoelezwa Profesa Safari yupo katika kesi gani, sambamba na barua ya wito.

Kuhusu Mchungaji Msigwa na Heche kusafiri, amesema kuna haja ya kusikia kutoka kwa washtakiwa wenyewe pamoja na kupata uthibitisho ikiwemo cheti kwa ajili ya kumbukumbu ya mahakama.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alieleza kutoridhishwa kuahirisha kesi hiyo kwa siku 20 na kuipanga kuendelea Septemba 24 hadi 27 na Oktoba 1 hadi 3, 2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527