MAKONDA: NI NJAA TU, VINGINEVYO NINGEANDIKA BARUA YA KUJIUZULU


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amekiri kudhalilishwa na watendaji wake wa chini hii ni baada ya Rais Magufuli kuonesha kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo machinjio ya Vingunguti na ufukwe wa Coco.

Makonda ameyabainisha hayo leo Septemba 17, 2019 katika hafla ya utoaji udhamini kwa Wanafunzi wa kike 100, wanaosoma masomo ya Sayansi kutoka katika familia zenye kipato cha chini, kwa madai ya kwamba amedhalilika mbele ya Mkuu wa nchi hali iliyomnyima raha hadi kutamani kuacha kazi.

''Jana ilikuwa aibu, jana nimedhalilika mimi, watendaji wangu jana mmenivua nguo na aibu ile imenifanya hata sijalala, usingizi sijapata kabisa mpaka nikawa najiuliza nakosea wapi? sababu tunakaa vikao vingi vya kutoa maelekezo mengi dhidi ya miradi ya maendeleo katika mkoa wetu'' amesema Rc Makonda.

Makonda amedai kuwa, njaa ndiyo inamfanya aendelee kushikilia nafasi hiyo.

''Yaani kwa sababu njaa tu ni kali, kama sio njaa kali leo ilipaswa mimi niwe nimeandika barua ya kuacha kazi, sasa ukiwaza kuacha kazi njaa hii, huko kwenu kwenyewe ulikotoka, kijijini kwetu Koromije hata majirani nishawasahau'' amesema Makonda.

Kufuatia hali hiyo Makonda ameunda kamati maalumu ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika mkoa huo, itakayohusisha TAKUKURU ili kuhakikisha aibu kama hiyo haijirudii tena.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Magufuli, kutembelea machinjio ya Vinguguti na kubaini ucheleweshwaji wa ujenzi wa machinjio hayo na kumuagiza Mkuu wa Mkoa pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, kuacha maneno na badala yake wahakikishe miradi inamalizika kwa wakati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527