Bashungwa: Mazingira Ya Uwekezaji Sasa Ni Mvuto Kwa Wawekezaji Wa Ndani Na Nje


Abraham Nyantori, MAELEZO
Wizara ya Viwanda na Biashara katika siku yake ya pili ya Kongamano la fursa za biashara baina ya Tanzania na Uganda imerudia kuwahakikishia wafanyabiashara wake kuwa Wizara yake itawahudumia kwa karibu kwa kila hatua ili kufanikisha lengo la kufanya biashara baina ya nchi hizi mbili. 


Akifunga Kongamano hilo leo, baada ya mjadala mrefu uliojumuisha wawekezaji, wafanyabiashara wa bidhaa, wasafirishaji na wajasiriamali katika Kituo cha Mikutano cha Julias Nyerere, Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, ametumia muda huo kusisitiza wafanyabiashra kutumia fursa ya maboresho ya sheria na mazingira ya biashara kuwekeza, ndani na wawekezaji wa nje. 


Waziri amewaeleza Waganda fursa zilizopo katika sekta za kilimo, madini, mali ghafi za mazao mbalimbali na bidhaa kwa walaji, na akawaeleza mazingira ya uwekezaji yamefanyiwa tafiti mbalimbali na serikali baada ya maboresho, mabadiliko  yametengenezewa nyaraka (blue print). 


Waziri amekiri kuwa majukwaa mbalimbali yamekuwa yakifanyika lakini shughuli zote zinaishia kubaki katika makabati pasipo utekelezaji, “sasa tunatakiwa kuongea kidogo na kufanya vitendo zaidi” amesisistiza waziri hasa kwa wafanya maamuzi, “kwa haya maamuzi tuliofikia nitatoka ofisini na kufuatilia kila moja kuona utekelezaji wake” ametahadharisha Waziri Bashungwa. 


Katika Kongamano la leo, baada ya wachokozaji wa maada kadhaa katika sekta ya usafirishaji na wa vipimo kumaliza,  washiriki wa Kongamano wamejikita katika eneo hilo muhimu huku wakieleza changamoto zinazokabili sekta za usafirishaji, pia, michakato ya usajili, ukakasi wa “njoo kesho” na kuwa baadhi ya wafanyamaamuzi huchukua muda mrefu kutekeleza ama kutoa vibali. 


Watendaji wa juu wa serikali za Uganda na Tanzania, wakiongozwa na Waziri wa Viwanda, ambaye mwenzake wa  Uganda  alikuwa na jukumu lingine hapa jijini walionesha umakini wa kuchukua mawazo na maswali ya washiriki wa Kongamano, na baadhi yao walipata nafasi ya kujibu maswali. 


Baadhi ya wafanyabiashara wasafirishaji walitaka kujua gharama za usafirishaji wa mzigo kutoka Mwanza/Uganda hadi Dar es Salaam, huku wakilinganisha na gharama za usafirishaji wa mzigo kama huo kutoka bandari ya Mombasa, Kenya; hata hivyo watendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) walisema bei zake zimeshushwa na mazingira yameboreshwa. 


Akichangia maada, Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damasi Ndumbaro, amekumbusha historia ya undugu wa nchi hizi mbili, na kuwa Uganda haijawahi kupigana na Tanzania, akasema, “Vita ya Kagera 1977 ilikuwa ni mjumuisho wa Waganda na Watanzania kuondoa utawala wa kidikteta wa nduli Idd Amini, nchini Uganda. 


Waziri akakumbusha kuwa huduma ya TRC toka Dar es Salaam hadi Uganda huchukua siku tatu tu baada ya kuondolewa baadhi ya vikwazo, na reli ya kisasa ya mwendo kasi ikamilikapo safari hiyo itakuwa ya siku moja, pia akahimiza Waganda na Watanzania kuunganisha nguvu zao na kuliingia soko la Sudan. 


Kwa upande mwingine, Naibu Waziri huyo akaeleza masikitiko yake ya nchi za kiafrika kuendelea kutumia lugha za kikoloni kama lugha rasmi za vikao vya kimataifa, akasema. “lugha pekee isiyo ya kabila fulani na isiyo lugha ya kikoloni ni Kiswahili, … tubadilike, tuwe na lugha ya kutuunganisha, nayo ni Kiswahili.” 


Akasema, “Natetea kiswahili kwa sababu sio lugha ya kabila lolote, ni lugha ya pili baada ya kiarabu katika bara la Afrika…. Ni lugha ya kumi katika mlolongo wa lugha za kimataifa, hii ni silaha kubwa kwetu, tusiendelee kutukuza tamaduni za wenzetu kwa kudharau zetu.”
    


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post