MTOTO WA MIAKA 7 AUAWA KWA KUPIGWA NA BABA YAKE KISA KUPOTEZA NG'OMBE AKIWACHUNGA







Na Walter Mguluchuma - Malunde 1 blog

Picha haihusiani na habari hapa chini
Mtoto aitwaye  Lusambaja Bundala(7) Mkazi wa Kitongoji cha Luhafwe Kata ya Ntongwe Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi  ameuawa kwa kupigwa kichwani na kukatwa na kitu chenye ncha kali na anayedaiwa kuwa  baba yake mdogo baada ya mtoto huyo kupoteza ng'ombe aliokuwa akiwachunga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Benjamin Kuzaga alisema kuwa tukio hilo limetokea Septemba 16,2019 majira ya saa nne asubuhi katika kitongoji cha Luhafwe wilaya ya Tanganyika.

Alieleza kuwa wakati wa uhai wake, marehemu alikuwa akiishi nyumbani kwa baba yake mdogo aitwaye Juma Lusambaje (28) ambaye ndiyo mtuhumiwa wa mauaji hayo.

"Kabla ya kuuawa kwa mtoto huyo,Septemba 12,2019 marehemu akiwa na mtoto mwenzake aitwaye Ibrahimu Lusambaja(13) walitumwa na mtuhumiwa kwenda kuchunga ng'ombe. Tangu siku hiyo hakuonekana hadi hapo jana majira ya saa nne asubuhi alipokutwa akiwa amefariki dunia kwa kuuawa kwa kupingwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kuchomwa na kisu chini ya kidevu",ameeleza Kamanda Kuzaga.

Kamanda Kuzaga amesema chanzo cha mauaji ya mtoto huyo ni hasira za mtuhumiwa baba yake mdogo Juma Lusambaja kuchukia baada ya marehemu kupotelewa na ng'ombe aliokuwa anachunga.

"Baada ya marehemu kupoteza ng'ombe ndipo mtuhumiwa alipoamua kuchukua sheria mikononi na kuamua kumpiga mtoto kwa kutumia chuma chenye ncha kali na kumchoma na kisu hadi kumuua na hakutoa taarifa kwa mtu yeyoye",ameongeza.

Amesema Mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani ili akajibu tuhuma zinazo mkabili 

Mwili wa marehemu umekabidhiwa ndugu wa marehemu kwa ajiri ya mazishi baada ya kuwa umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527