MAMLAKA YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA NISHATI NA MAJI (EWURA) YATANGAZA BEI MPYA ZA PETROL NA DIZELI....SOMA HAPA

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) nchini Tanzania imetangaza bei za kikomo kwa bidhaa za mafuta nchini humo zitakazoanza kutumika kuanzia leo Jumatano Septemba 4,2019.


Taarifa iliyotolewa  Jumanne Septemba 3,2019 kwa vyombo vya habari na mkuu wa kitengo wa mawasiliano na uhusiano kwa umma wa Ewura, Wilfred Mwakalosi amesema bei za jumla na rejareja za mafuta za petroli dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka.

Mwakalosi amesema mafuta hayo ni yale yaliyoingia kupitia bandari ya Dar es Salaam ambayo yameongezeka ukilinganisha na mwezi uliopita.

“Mwezi huu (Septemba) bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa Sh83 kwa lita (sawa na asilimia 3.87), Sh61 kwa lita (sawa na asilimia 2.90), Sh46 kwa lita (sawa na asilimia 2.22),” amesema

Amesema bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na yanayoingizwa kupitia bandari ya Tanga yameongezeka ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.

“Kwa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara mwezi huu bei zimeongezeka kwa Sh108 kwa lita sawa na asilimia 4.95 na  Sh72 (sawa na asilimia 3,36),” amesema Mwakalosi.

Katika taarifa hiyo, Mwakalosi amesisitiza bei ya mafuta ya taa kwa mikoa ya kaskazini zitaendelea kutumika zile zilizochapishwa mwezi uliopita kwa sababu hakuna shehena ya bidhaa hiyo iliyoingia kupitia bandari ya Tanga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527