Breaking : RAIS MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA MKUU WA WILAYA NA MKURUGENZI WAKE WALIOGOMBANA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro,Majura Mateko Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Malinyi,Mussa Elias Mnyeti leo Jumanne Septemba 17,2019.
Uteuzi wa viongozi watakaojaza nafasi hizo utajazwa baadae.
Jana Jumatatu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza kuchukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mussa Mnyeti, hivyo kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji kazi wao.

“Ni aibu Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amewateua vijana wawe viongozi lakini leo hadi wananchi wa kawaida wanajua mgongano wenu maofisini. Ni aibu Mkuu wa Wilaya ya Mkurugenzi mnagombana tena wakati mwingine mnagombania miradi, mmesahau kutekeleza majukumu yenu.”

Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo (Jumatatu, Septemba 16, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Toboa, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Alisema Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya wananchi na inapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya jamii kama kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara lakini wao wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.

Waziri Mkuu amesema mbali na CAG na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza utendaji wa viongozi hao, pia ameuelekeza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakakague miradi ya ujenzi inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo kama ubora wake unalingana na thamani halisi.” Baada ya kupata majibu ya uchunguzi na kubaini kiini cha tatizo ndani ya wilaya hii hatua zitachukuliwa.”

Awali, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dkt. Haji Mponda alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwenye wilaya hiyo kuna matatizo ya mahusiano kati ya Serikali na Halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.

Mbunge huyo alisema kutoelewana kwa viongozi wa wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kumesababisha mgawanyo mkubwa kuanzia katika Baraza la Madiwani hadi kwa wananchi mitaani, hivvyo alimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika. Kilipatia ufumbuzi suala hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527