WAZIRI UMMY AZIKARIBISHA NCHI ZA SADC KUTIBIWA MUHIMBILI, MOI


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu  amezikaribisha nchi wanachama wa SADC kutumia huduma za ubingwa wa juu zinazopatika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Ummy ameyasema hayo jana alipotembelea  mabanda ya MNH, MOI na JKCI yanayoshiriki maonesho ya viwanda yanayofanyika katika viwanja vya ukumbi  wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kuelekea mkutano mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao utaanza mapema wiki hii.

Waziri Ummy amesema Wizara yake imeweka wataalam wa afya ili kutoa huduma kwa wajumbe wa mkutano wa SADC watakaohitaji huduma za matibabu pamoja na wananchi wengine watakaokuwapo katika viwanja hivyo.

Aidha ameziomba nchi za SADC kupata huduma za ubingwa wa juu zinazopatikana MNH kama upandikizaji figo (kidney transplant), upandikizaji watoto vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant), tiba kwa njia ya radiolojia (interventional radiology).

Kwa upande wa MOI, Waziri Ummy amezitaka nchi za SADC kuja kupata huduma za upasuaji wa mivunjiko ya kikombe cha mfupa wa nyonga, upasuaji wa kuweka nyonga na magoti bandia na upasuaji wa magoti, ubongo na mgongo kupitia matundu madogo.

Kwa upande wa JKCI amezitaka nchi za SADC kupata huduma za tiba ya umeme wa moyo, kuzibua mishipa ya damu na upasuaji wa kufungua kifua kwa ajili ya kurekebisha valvu au matundu kwenye moyo.

 “Kama Wizara tumeweka wataalam wa afya hapa eneo la mkutano  ili kutoa huduma kwa wajumbe wa nchi za SADC. Wataalam wetu wa Muhimbili, MOI, JKCI na pamoja  Hospitali ya Lugalo wako tayari kuhudumia wageni wetu ambao watapata changamoto yoyote ya kiafya,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ametembelea kliniki maalumu zilizoandaliwa kwa ajili ya kuhudumia wageni na wananchi mbalimbali wanaotembelea maonesho ya viwanda na maandalizi ya mkutano wa 39 wa SADC.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527