WAZIRI SIMBACHAWENE APONGEZA MRADI WA UPANDAJI MIKOKO ZANZIBAR

Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. George Boniface Simbachawene ameupongeza mradi wa utunzaji mazingira kupitia upandaji miti ya mikoko mjini Zanzibar.

Mhe. Simbachawene ametoa pongezi hizo Agosti 5, 2019 katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kujitambulisha na kukagua miradi ya Muungano na Mazingira visiwani hapa.

Akiwa katika eneo hilo lenye hekta nne lililopo Shehia ya Kilimani Wilaya ya Mjini Mkoa wa Magharibi alisema ameridhishwa kuona namna ambavyo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ilivyotekeleza mradi huo pamoja na ufadhili kutoka Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

“Niwapongeze sana kwa mradi huu mzuri na tunaona matokeo yake umesaidia mawimbi yasije kwa kasi katika eneo hili na kusababisha mmonyoko na tukiamua kufanya kazi kwa pamonja na jamii tunaweza kufanya vizuri,” alisema.

Aidha, Mhe. Simbachawene alitoa wito kwa wataalamu kuangalia namna ya kuibua miradi mingine katika fukwe za mikoa mingine kama Dar es Salaam, Tanga, Lindi na Mtwara ili kusaidia kutunza mazingira.

Katika hatua nyingine alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kianga katika Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi aliwapongeza wananchi kwa kusimamia mradi huo.

Alisema kuwa kwa kiasi cha sh. milioni 174 inadhihrisha namna wanavyotumia fedha kwa uaminifu na kuwa tutapiga hatua katika kuendeleza sekta ya huduma ya afya kwa wananchi.

“Nawapongeza sana wananchi hasa kwa kamati hii mmefanya vizuri kusimamia mradi huu wa ujenzi wa kituo cha afya tunaamini udokozi haukuwepo kazi imefanyika fenicha (samani) zipo, vifaa tiba na utendaji kazi mzuri unaendelea kufanyika,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527