WAZIRI KALEMANI: BADO TUNAHITAJI GESI ZAIDI ITAKAYOSAIDIA KUIMARISHA UCHUMI WA VIWANDA

Na Veronica Simba – Dar es Salaam

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, amesema pamoja na kwamba Tanzania imeshagundua gesi futi za ujazo trilioni 57.54 hadi sasa, bado inahitaji gesi zaidi itakayosaidia kuimarisha uchumi wa viwanda.

Aliyasema hayo jana Agosti 3, 2019 jijini Dar es Salaam, alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Alisema, kazi ya utafutaji wa gesi inaendelea vizuri lakini akaisisitiza Menejimenti hiyo kuongeza kasi zaidi katika utafutaji wake pamoja na wa mafuta.

“Mahitaji ya gesi ni makubwa. Tunahitaji gesi kuzalisha umeme, tunahitaji gesi ya kutosha kwa matumizi ya majumbani na pia viwandani,” alieleza.

Aidha, Waziri aliitaka Menejimenti husika kutafuta mbinu mbalimbali na kuongeza ubunifu ili shirika hilo liweze kufanya biashara kiushindani, lipate mapato na baadaye lianze kutoa gawio serikalini.

Akifafanua, alisema, mwaka 2015 ilipitishwa sheria mpya ya mafuta ambayo ilibadili majukumu ya shirika kutoka kutegemea ruzuku ya serikali na kuwa shirika lenye kujiendesha kibiashara.

“Sasa, TPDC ikiwa ni kampuni ya serikali yenye kufanya biashara, ni lazima ifanye biashara kiushindani.”

Waziri alilitaka shirika hilo kupanua wigo wa usambazaji gesi majumbani hususan mkoa wa Dar es Salaam ambao una watumiaji wengi wa nishati ya mkaa, inayosababisha ukatwaji wa miti kwa kiwango kikubwa.

Vilevile, alitaka viwanda vingi zaidi viunganishiwe mfumo wa gesi kutoka 40 vilivyopelekewa huduma hiyo, ili kuvipunguzia gharama ya uzalishaji inayotokana na matumizi ya nishati nyingine.

Kwa upande wa matumizi ya gesi kwenye magari, Dkt Kalemani aliiagiza TPDC ifungue vituo zaidi vya kujazia gesi katika mikoa mbalimbali ili wateja walioko mikoani wapate huduma ya kubadili mfumo wa magari yao kutoka ule unaotumia mafuta na kuweka unaotumia gesi, ili kuwaepushia usumbufu wa kufuata huduma hiyo Dar es Salaam ambako ndiko kuna kituo pekee kwa sasa.

Aidha, alilitaka shirika hilo kuvifufua vituo vyake sita vya mafuta na kuongeza vingine zaidi ili iendeleze biashara hiyo kama wanavyofanya PUMA na wengine kwa ajili ya kuongeza mapato yake.

Maagizo mengine aliyotoa Waziri kwa Menejimenti hiyo ni kuandaa utaratibu wa kuachana na uagizaji nje ya nchi vifaa mbalimbali vya kusambazia gesi zikiwemo mita na mabomba, badala yake itumie vile vitakavyozalishwa nchini.

“Hii itawezesha viwanda vya aina hiyo kujengwa hapa nchini, watanzania watapata ajira na pia itarahisisha zoezi la kusambaza gesi maana vifaa vitakuwa vikipatikana nchini.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. James Mataragio, alimhakikishia Waziri kuwa shirika lake litatekeleza kikamilifu maagizo yote aliyowapatia.

“Tayari tumeshaanza kujipanga katika maeneo yetu ya kazi yanayojumuisha utafiti, uzalishaji  na biashara ya gesi. Nimerudi nikiwa na nguvu mpya kuwatumikia watanzania,” alisema Dkt Mataragio ambaye amerudishwa katika nafasi hiyo na Rais John Magufuli hivi karibuni, baada ya kusimamishwa kwa muda.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara akiwemo Katibu Mkuu, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo pamoja na Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi Adam Zuberi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527