WAZIRI JAFO AZIAGIZA HALMASHAURI ZOTE NCHINI KUWA WABUNIFU WA MIRADI YA MAENDELEO


Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaweka mikakati kwa kubuni miradi ambayo itawasaidia katika kujiwekea vitega uchumi na kukuza mapato katika Halmashauri zao ili kuachana na utegemezi katika Serikali.

Ameyasema hayo leo wakati wa utiaji wa saini Miradi ya Ujenzi wa majengo mawili ya vitega uchumi vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square, Jijini Dodoma.

Mhe. Jafo amesema Halmashauri zote nchini zinatakiwa kuwa wabunifu, kujipanga na kuweka mikakati ya kuondokana na unyafuzi wa mapato kwa kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuongeza mapato na kuleta maendeleo kwa jamii.

Amesema kuwa kama Halmashauri zote zingekuwa wabunifu na kuamua kujitoa katika utendaji kazi kusingekuwa na unyafuzi wa mapato bali zingejikita katika kubuni na kuibua miradi ya maendeleo ili kujikwamua kiuchumi na kujiongezea vitega uchumi vitakavyoleta maendeleo katika Halmashauri zao.

“ Kusipokuwa na ubunifu, kujitoa katika utendajikazi wa watumishi wa Halmashauri, hali ya unyafuzi wa mapato itaendelea na bado Halmashauri nyingi zitakuwa ni tegemezi kwa Serikali, hivyo ninaziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanabuni vitega uchumi ili waweze kujitegemea
kwa kutumia mapato yao ya ndani ” Anasisitiza Mhe.Jafo.

Mhe. Jafo amezitaka Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kubuni Miradi ya Maendeleo kwa ajili ya vitega uchumi na kuondokana na utegemzi kwa Serikali.

Amefafanua zaidi kuwa watumishi wa Serikali za Mitaa nchini kuacha kufanyakazi kwa maigizo, kwa kujionyesha kwenye mitandao bali wafanyekazi kwa weledi lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi maskini na kulipeleka taifa katika uchumi wa kati.

“Kuna watu nchi hii wamezoea maigizo, hivyo kwa wale ambao wapo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuacha kufanyakazi kwa maigizo bali watu wafanyekazi kwa weledi ili kufikia mallengo ya Serikali.” Amesisitiza Mhe. Jafo.

Amesema watu wasipende kujionyesha kwenye mitandao kuwa wanafanyakazi , bali wafanye kazi kwa ajili kulitumikia taifa hasa wananchi maskini kwa kuwa nchi hii inabadilika na kinachohitajika ni maendeleo ya Taifa.

Amewasii vijana waliopewa dhamana ya uongozi nchini kufanyakazi kwa bidii na maarifa waliyonayo na kuacha kufanyakazi kwa maigizo, lengo likiwa ni kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli katika kufikia uchumi wa kati.

Amewapongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuweza kutumia Makusanyo ya Fedha za Ndani kwa ajili ya ujenzi wa vitega uchumi lengo kubwa ni kutoa unyafunzi wa mapato na kupunguza utegemezi kwa Serikali.

Wakati huohuo Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi amesema ujenzi wa jengo la Hoteli “Dodoma City Hotel” litajengwa katika eneo la Paradise barabara ya Nyerere kwa gharama ya shilingi bilioni 9.9 kutoka katika nyanzo vya mapato ya ndani lengo likiwa ni kupunguza utegemezi kwa Serikali, kuongeza ajira kwa wananchi wa Dodoma, kutoa huduma bora kwa wananchi, kuboresha mji wa Dodoma na kupunguza umaskini na kuongeza kipato kwa wananchi wa Dodoma.

Bw. Kunambi ameendelea kusema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inategemea kujenga kitega uchumi Mji wa Serikali “Government City Complex “kwa gharama ya shilingi bilioni 59.3 ambapo kutakuwa na ofisi, maduka,Kumbi za Mikutano, Maegesho ya Magari, Maeneo ya mabenki, migahawa bna maeneo ya mahoteli.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge amesema kuwa kupitia miradi hiyo Wananchi wa Mkoa wa Dodoma watapata fursa ambazo zitawasaidia kuongeza kipato na kukuza uchumi wa Dodoma utaongezeka.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527