KATIBU MKUU WA CCM AMPONGEZA ASKARI POLISI ALIYEGOMA KUSEMA 'KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI"

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Dk Bashiru Ally amempongeza askari polisi wa mkoani Pwani ambaye siku za hivi karibuni aligoma kutumia salamu ya ‘Kidumu Chama cha Mapinduzi’ inayotumiwa na chama hicho tawala nchini Tanzania.

Askari huyo aliombwa kutoa salamu hiyo na mjumbe wa halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho, Haji Jumaa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Vianzi wilayani Mkuranga, kabla ya kueleza kero za kufungwa kituo cha polisi muda wa kazi.

Hata hivyo, askari huyo aligoma akisema maadili ya kazi yake hayaruhusu kutoa salamu hiyo, akidai ni kosa kimaadili.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 27, 2019 katika mkutano wa wanachama wa CCM wilaya ya Ubungo ikiwa ni sehemu ya ziara yake iliyoanza leo ya kukagua uhai wa chama, miradi ya maendeleo na kuzindua mashina.

Akitoa mfano wa tukio hilo, Dk Bashiru amesema CCM haiwezi kuwa chombo cha nidhamu kwa watumishi wa umma.

"Nampongeza yule askari aliyegoma kufuata maelekezo nataka nimjue hata IGP nilimpigia simu kuhusu tukio hilo.”

"Polisi hapokei maelekezo ya chama chochote cha siasa iwe CCM au CUF. Kama una jambo usibwatuke tu, sitaki kusikia amri au maelekezo yoyote, tukiendelea na tabia hiyo tutakuwa tunajenga nchi isiyofuata sheria,” amesema Dk Bashiru.

Amebainisha kuwa watumishi wa umma wana vyombo vyao vya kuwajibishana na wakati mwingine hupeana adhabu.

Na Kelvin Matandiko Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post