WATATU WATIWA MBARONI KWA KUKUTWA NA VIPANDE 10 VYA MADINI BANDIA YA DHAHABU


Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kukutwa na vipande 10 vya madini bandia aina ya dhahabu wakiwa kwenye harakati za kuyauza wilayani Kahama.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Richard Abwao, alisema watuhumiwa hao walikuwa na mtambo wa kufyatua madini hayo bandia ya dhahabu ambayo huyauza wilayani Kahama, Geita pamoja na Mwanza.

Alisema katika misako ya uhalifu ambao waliufanya mwezi uliopita mkoani humo, walifanikiwa kukamata watuhumiwa 73 wa matukio mbalimbali ya uhalifu, wakiwamo wezi, wauaji, pamoja na watu watatu wa utengenezaji wa madini bandia ya dhahabu.

Alisema pia walifanikiwa kukamata watuhumiwa wanne waliohusika na matukio ya mauaji ya Kalekwa Shiku (50) mkazi wa kijiji cha Mishepo, Shinyanga vijijini, ambaye aliuawa kwa kufunikwa mfuko usoni, kufungwa mawe miguuni, na kisha kuzamishwa kwenye bwala la maji na kufariki dunia.

Alisema watuhumiwa hao walitekeleza mauaji hayo Juni 6, mwaka huu, kwa madai ya tamaa ya kutaka kujipatia ng'ombe tisa kwa mwanamke huyo na baada ya kugoma ndipo wakatekeleza mauaji hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527