WALIOFARIKI KWA AJALI YA MOTO MOROGORO WAFIKIA 100....DAKTARI AELEZA SABABU YA VIFO KUONGEZEKA


Idadi ya waliofariki kutokana na ajali ya moto wa lori la mafuta mkoani Morogoro, Agosti 10, 2019 imefikia 100.

Hii inatokana na majeruhi mwingine mmoja kufariki jana usiku Jumanne wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Kifo hicho kimekuwa cha tatu kwa siku ya jana Jumanne ambapo hadi saa 10 jioni ya jana Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kabwe alisema majeruhi wawili kati ya 18 walikuwa wamefariki dunia.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa MNH, Aminiel Aligaesha amewataja waliofariki ni Mazoya Sahani, Khasim Marjani na Ramadhani Magwila.

Amesema majeruhi waliobaki katika hospitali hiyo waliolazwa chumba cha uangalizi maalum (ICU) ni 13 na wawili wametolewa ICU na kulazwa wodi ya Sewahaji.

Daktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Laurian Rwanyuma amesema majeruhi wa ajali ya lori la mafuta iliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro wanaendelea kupoteza maisha kutoka na kuungua kwa asilimia 80 hadi 90.

Dk. Rwanyuma amesema majeruhi wengi waliopelekwa hospitalini hapo, waliungua zaidi sehemu za ndani kama vile mfumo wa hewa na figo hivyo kusababisha kupumua kwa shida.

“Kutokana na ngozi zao kuungua kwa asilimia kubwa hali hiyo imesababisha mwili kukosa kinga na kupoteza maji mengi.

“Kwa kawaida wagonjwa walioungua kiasi hicho wana uwezekano mdogo wa kupona hata kama hospitali ina uwezo mkubwa wa vifaa na madawa,” amesema.

Hata hivyo, amesema wanaendelea kufanya juhudi za hali ya juu ili majeruhi waliobaki waweze kupona.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post