SERIKALI YAWATAKA WACHAWI KUSITISHA SHUGHULI ZAO USIKU ILI WAHESABIWE


Wachawi wa kukimbia usiku Kaunti ya Homa Bay nchini Kenya wametakiwa kufunga biashara yao kwa siku mbili ili kuruhusu zoezi la sensa kufanyika bila ya kutatizwa.

 Serikali imewataka kukaa ndani usiku hadi zoezi hilo lililoanza Jumamosi, Agosti 24 litakapokamilika asubuhi ya Jumatatu, Agosti 26,2019. 

Harman Shambi ambaye ni Kamishna wa Kaunti ya Homa Bay, aliwataka wachawi kujizuia kutoka usiku ili nao pia wahesabiwe 

Shughuli za wachawi katika maeneo mengi ya humu nchini hufanywa usiku, na sarakasi zao huwa ni za kutisha mno; miongoni mwazo ni kutimka mbio na kuparamia miti katika maboma ya watu, kurusha mawe na mchanga kwenye paa na ndani ya nyumba, kuacha vinyesi katika maboma ya walengwa wao miongoni mwa nyinginezo nyingi. 

“Ni Wakenya na hivyo ni lazima kuhesabiwa. Kwa hivyo ni lazima kujizuia kutoka usiku ili wahesabiwe,” alisema na kunukuliwa na Nation, Jumamosi, Agosti 24,2019.

 Kauli yake ilifuatia ujumbe wa Twitter uliotamba sana wiki hii uliodai Waziri wa Usalama wa Ndani Dk Fred Matiangi amepiga marufuku shughuli za wachawi wote wa usiku kaunti za Homa Bay na Kisii wakati wa sensa.

“Matiangi awaonya wachawi wote kaunti za Kisii na Homa Bay awataka waheshimu serikali na wasitoke nje kwa siku kadhaa. Wachawi wote sharti kuhesabiwa ,” ujumbe huo ulisema. 

Shambi pia aliwaonya watu wanaopanga kujifanya ni maafisa wa sensa ili kuwahangaisha watu kwamba, watachukuliwa hatua kali za kisheria, aliwataka raia kuwa makini na kuchukua tahadhari za mapema. 

“Maafisa wa sensa watajitambulisha na watachomoa baji zao ma jaketi zao za kumwe kwenye mwangaza. Wataandamana na machifu na wazee wa vijiji ili kuifanya kazi hiyo kuwa rahisi,” alisema. Hata hivyo zoezi hilo linatazamiwa kuendelea kwa siku saba baada ya kufungwa rasmi usiku wa kuamkia Jumatatu.
Chanzo - Tuko

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527