WATOTO,WANAFUNZI ZAIDI YA LAKI 2 KUPATIWA VYETI VYA KUZALIWA KAHAMA


Mtendaji mkuu wa wakala wa usajili ufilisi na udhamini(RITA) Emmy Hudsoni

Na Salvatory Ntandu - Malunde1 blog Kahama

Zaidi ya watoto 200,000 wenye Umri kati ya miaka mitano hadi 18 wakiwemo wanafunzi katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wanatarajiwa kupatiwa vyeti vya kuzaliwa wakala wa usajili ufilisi na udhamini(RITA).

Hayo yamebainishwa leo Mtendaji mkuu wa wakala wa usajili ufilisi na udhamini(RITA) Emmy Hudsoni kwenye mafunzo ya siku moja kwa waratibu elimu kata na Maafisa elimu kutoka halmshauri za Ushetu,Msalala na Kahama Mji yaliyofanyika wilayani humo.

Amesema vyeti vya kuzaliwa kwa watoto na wanafunzi ni haki ya msingi kwao hivyo ni budi kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawasajili ili waweze kupatiwa katika kampeni hii maalumu ambayo itafanyika katika kata zote zilizopo katika wilaya ya kahama.

Naye Victoria Lembeli mjumbe wa bodi ya (RITA) amewataka waratibu elimu na walimu kufanya kazi kwa weledi na uzalendo mkubwa kwani zoezi hilo linawahusu watoto wa raia wa Tanzania pekee.

Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo,Tumshukuru Mdui na Helena Alex wameiomba serikali kutoa elimu kwa wananchi ili watambue umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa.

Awali akizungumza Mkuu wa wilaya ya kahama Anamringi Macha aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mafunzo hayo amesema atahakikisha analisimamia zoezi hilo kwa umakini mkubwa na kutembelea Halmashauri zote za Msalala, Ushetu na Kahama mjini ili kuhakikisha wanaosajiliwa kuwa ni watanzania pekee.

Ameongeza kuwa uwepo wa kampeni hiyo itasaidia kupunguza msongamano katika Ofisi yake kwani zoezi litaweza kuwafikia wananchi moja kwa moja kwenye kata zao.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527