WANACCM WATAKIWA KUPENDANA NA KUSHIKAMANA ILI WASHINDE KWA KISHINDO KWENYE UCHAGUZI

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Buganzo kata ya Ntobo halmashauri ya Msalala na kukemea kuwepo na makundi ndani ya CCM hasa kuelekea kwenye kipindi cha uchaguzi, na kuwataka wawe kitu kimoja ili ushindi uweze kupatikana kwa kushinda viti vyote. Picha na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Na Annastazia Paul - Malunde1 blog

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameaswa kushirikiana, kupendana na kushikamana ili kukiwezesha chama hicho kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao.

Rai hiyo imetolewa leo  Jumatatu Agosti 19,2019 na Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la Msingi katika jengo la ofisi ya CCM tawi la Bunganzo kata ya Ntobo Wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Balozi Iddi amesema  migogoro na makundi hayana tija badala yake yanaharibu mambo ndani ya chama hicho.

Katika hatua nyingine amewataka makatibu wa wilaya kutokuwa na upendeleo katika uteuzi wa wagombea.

"Makatibu wa wilaya baadhi yao wanapenda sana kupendelea na kubeba beba hivyo wasifanye hivyo kwani wao ndiyo waamuzi, wawapime tu huyu anafaa kwa kigezo kipi, ili kupata ushindi mzuri katika chama chetu",amesema Balozi Iddi.

Pia amewaomba wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwani ushindi hauwezi kupatikana kama watu hawajajiandikisha.

"Agosti 26 mwaka huu hadi Septemba 1,2019 watu wote mkoani Shinyanga wenye sifa za kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kurawaende kwa wingi ili wapate sifa za kupiga kura kwani bila kufanya hivyo hawataweza kupiga kura, na siku ya kupiga kura wote wajitokeze ili wakapige kura katika ngazi zote kwani kujiandikisha pekee haitoshi",ameongeza.

Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kesho  Jumanne Agosti 20,2019 ataendelea na ziara yake wilayani Kahama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post