SERIKALI: UHALIFU WAPUNGUA NCHINI


Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu nchi imeendelea kuwa katika amani na utulivu huku uhalifu ukipungua kwa asilimia 2.2 kwa makosa makubwa ya jinai ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita hali inayopelekea wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi kwa amani na usalama.Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati akisoma taarifa ya Serikali mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliyohusu Hali ya Ulinzi na Usalama wa Raia na Mali zao kwa Kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu ikiwemo utekelezaji wa dhana ya Ulinzi Shirikishi.

“Kuanzia Januari hadi Juni ndani ya mwaka huu jumla ya makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi nchi nzima yalikuwa 28,252 tofauti na kipindi kama hiki mwaka uliopita ambapo makosa 28,889 yaliripotiwa vituoni, tukiangalia vizuri hesabu zetu ndani ya mwaka huu tumepunguza makosa 637 hii yote inatokana na juhudi za askari wetu na utekelezaji wa dhana ya ulinzi shirikishi” alisema Masauni

Naibu Waziri Masauni ameyataja makosa hayo makubwa ya jinai kuwa ni Makosa dhidi ya binadamu, Makosa dhidi ya Maadili ya Jamii, Makosa ya kuwania mali na Makosa ya Uhalifu wa Kifedha

Akizungumzia makosa ya usalama barabarani Naibu Waziri Masauni amesema kumekuwepo na mafanikio katika kupunguza makosa ya usalama barabarani hali inayochagizwa na usimamiaji wa sheria na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu..

“Takwimu za makosa ya ajali za barabarani katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu zinaonesha kuwepo kwa jumla ya makosa 1,610 yaliyoripotiwa ikilinganishwa na makosa 2,200 mwaka uliopita huku takwimu zikiweka wazi makosa 590 kupungua katika vipindi hivyo viwili” alisema Masauni

Alisema kutokana na kupungua kwa makosa ya barabarani hata idadi ya ajali zilipungua hali iliyopelekea kupungua kwa vifo kwani mwaka jana watu 1,051 walifariki tofauti na mwaka huu ambapo kuanzia mwezi Januari mpaka Juni watu 781 walipoteza maisha.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro alisema mafanikio hayo ya kupungua kwa uhalifu nchini yamechangiwa pia na matumizi ya teknolojia katika kupambana na uhalifu huku akiwaonya wahalifu kutafuta shughuli nyingine ya kufanya.

“Tunatumia vifaa maalumu ikiwepo drones katika kudhibiti uhalifu japo kwasababu za kiintelijinsia hatuwezi kusema ziko ngapi na maeneo gani muhimu tunawaasa wahalifu kuacha mipango yao ya kuvuruga amani ya nchi hii nawahakikishia hawatabaki salama,tunataka wananchi wafanye shughuli zao za kiuchumi” alisema IGP Sirro

Vikao vya Kamati za Bunge zinaendelea jijini Dodoma huku wizara mbalimbali zikiwasilisha taarifa zao kwa kamati hizo huku vikao vya Bunge vikitarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post